Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
ENDAPO Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,
itaendelea kupuuzia na kufumba macho juu ya usimamiaji na ujenzi bora wa miradi
ya kilimo cha umwagiliaji, hakika maendeleo katika sekta ya kilimo hicho cha
umwagiliaji hapa wilayani yataendelea kudorola.
Siku zote jamii imekuwa ikitambua kilimo ni sekta
muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote ile hapa duniani na ni tegemeo kwa
wataalamu husika waliopo katika sekta hiyo, kuendeleza miradi mbalimbali ya
kilimo hicho, ili wananchi wake hususani wakulima waweze kuzalisha mazao yao shambani kwa ubora
unaokubalika.
Mwandishi wa makala haya anaelezea juu ya utata uliopo
katika mradi wa umwagiliaji wa Sangamabuni uliopo kijiji cha Mabuni kata ya
Litumbandyosi, ambapo umekuwa ukizua malalalamiko kutoka kwa wananchi kwamba
ujenzi wake unashindwa kuendelea kutokana na uongozi wa wilaya hiyo, kushindwa
kusimamia kikamilifu na kufuata taratibu husika za wataalamu wa kanda ya umwagiliaji
Mtwara.
Kana kwamba hilo halitoshi baadhi ya miradi mingi ya
kilimo cha umwagiliaji wilayani Mbinga, imejengwa kwa kiwango cha chini kiasi
ambacho kimekuwa kikisababisha serikali kuendelea kuingia gharama ya kuijenga
upya, kutokana na miundombinu iliyojengwa kusombwa na maji.
Uchunguzi ambao umefanywa na mwandishi wa habari hizi, juu ya mradi huo
wa Sangamabuni umebaini kwamba, mkandarasi aliyepewa jukumu la kuujenga ni GS
Company Limited, alisaini mkataba wa ujenzi huo mnamo Agosti 29 mwaka jana, na
kupata kibali rasmi cha kuanza kazi ya ujenzi Novemba 22 mwaka jana baada ya
kushinda zabuni.
Lakini tokea mkandarasi huyo apewe idhini ya kufanya
kazi hiyo hadi leo hii mradi huo unashindwa kusonga mbele, na badala yake
katika eneo la ujenzi wa mradi, mkandarasi amesogeza mawe tu na hakuna kazi
inayoendelea.
Wakulima walitegemea msimu wa mwaka huu waanze
kuzalisha mpunga, hivyo kutokana na mkandarasi huyo kutokamilisha kazi yake kwa
wakati wamebakia kwenye sintofahamu, na hawajui wafanye nini licha ya
malalamiko yao kuwepo mezani mwa viongozi wa wilaya ya Mbinga.
Kwa mujibu wa vyanzo vya uhakika vimesema kuwa mradi
huu tokea mkandarasi huyo apewe jukumu la kuujenga, kazi hiyo ilitakiwa iwe imekamilika
kwa muda wa miezi sita tokea aliposaini mkataba husika, lakini hali bado
imekuwa tete na siku za ujenzi zinakaribia kwisha.
Takribani miezi mitano sasa imepita utekelezaji wa
mradi huu umekuwa ni utata mtupu, ambapo nimeshuhudia jinsi gani ulivyo jambo
ambalo limenifanya leo hii nifikie hitimisho kwa nafasi hii kuelezea katika
makala haya.
Kwa ujumla jambo la msingi lililonigusa katika hili ni
kwamba utekelezaji wa mradi huu umegubikwa na madudu ambayo yanasababishwa na
baadhi tu ya wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, ambao awali walipewa
jukumu la kwenda kuupima na baadaye ufanyike usanifu na ujenzi wa miundombinu
ya umwagiliaji yaani ujenzi wa mifereji ya kupeleka maji mashambani, kazi
ambayo walishindwa kuifanya kutokana na kukosa utaalamu wa ujenzi wa miradi ya
umwagiliaji.
Mtandao huu umebaini kwamba timu ya watu watano kutoka
halmshauri ya wilaya hiyo, ilimwandikia barua Mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya wilaya ya Mbinga kumuomba gharama za uchunguzi na upimaji wa
mradi huo wa umwagiliaji Sangamabuni na mkurugenzi huyo aliwalipa fedha za
kujikimu(posho) na mafuta kwa ajili ya kuweka kwenye gari na kufikia jumla ya
shilingi milioni 2,130,0000 ili waweze kwenda huko kwa ajili ya kufanya kazi
hiyo.
Barua hiyo ni ya tarehe 11 Februari 2010 ambayo nakala
yake tunayo, yenye kumbukumbu namba MBWD/GF/II/Vol III/MM/28 ambayo ililenga
kumuomba mkurugenzi atoe fedha hizo huku ikiwa na majina ya wataalamu kutoka
idara ya maji na kilimo wilayani humo na kiasi cha fedha kwa kila mtumishi
aliyelipwa ambao ni Amos Mtweve aliomba kulipwa shilingi 270,000, Mohamed
Machela 420,000, Christomus Nchimbi 420,000, Alphonce Nakitundu 210,000 na
Vincent Buriani 300,000 ambapo walipewa na mafuta aina ya dizeli lita 300 yenye
thamani ya shilingi 510,000 kwa ajili ya kuweka kwenye gari ambalo liliwapeleka
huko katika kijiji cha Mabuni ambako mradi huo upo.
Kwa mujibu wa barua hiyo inasema gharama hizo ni kwa
ajili ya shughuli za upimaji tu na gharama za usanifu zitakuja baada ya upimaji
kufanyika, jambo ambalo linashangaza kwamba fedha hizo wamelipwa na kazi hadi
leo inaendelea kusuasua.
Pamoja na mambo mengine uongozi wa kijiji hicho
unasema wataalamu hao walishindwa kufanya kazi hiyo ya upimaji, na kufikia
hatua ya kumuomba injinia wa kanda ya umwagiliaji Mtwara Pius Makaka na
wenzake, kwenda huko na kulazimika kufanya kazi hiyo ya upimaji ambayo
iligharimu shilingi milioni 16 ambazo halmashauri hiyo inalojukumu la kuwalipa
kutokana kazi waliyoifanya ya upimaji.
Imebainika kuwa hadi sasa wataalamu hao wa kanda ya
umwagiliaji Mtwara baada ya kufanya kazi hiyo, inadaiwa wamelipwa kwanza shilingi
milioni 9 kati ya hizo na zilizobakia wanaendelea kuidai halmashauri hiyo.
Baada ya kukamilisha michoro ya upimaji huo injinia
huyo alileta gharama ya mradi huo kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya ya Mbinga, shilingi milioni 574 ambazo zinaweza kukamilisha ujenzi wa
mradi huo.
Gharama hizo zilipowasilishwa mezani kwa mkurugenzi
huyo wataalamu wawili kutoka idara ya maji na ujenzi katika halmashauri hiyo,
waliandika andiko la kuomba fedha katika ubalozi wa Japan hapa nchini, ambapo walifanikiwa
kupewa msaada wa shilingi milioni 275 ili waweze kuanza kazi ya ujenzi huo.
Fedha hizo zilipotolewa ndipo tenda ya ujenzi huo
ilipotangazwa na kufikia hatua ya kampuni ya GS kushinda zabuni husika, lakini
utata uliopo inadaiwa kwamba kikwazo kinachosababisha mradi huo usiweze
kujengwa kwa wakati unatokana na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga,
kutotaka kufuata taratibu za kitaalamu za michoro iliyochorwa na injinia wa
kanda ya umwagiliaji Mtwara na kulazimisha kutaka kufanya mambo kienyeji.
Wakati hilo likiendelea, injinia wa kanda baada ya
kuona siku zinazidi kwenda na mkandarasi husika tokea apewe jukumu la ujenzi wa
mradi huo hakuna kitu kinachoendelea, alimwandikia barua mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri hiyo ya terehe 3 Oktoba 2012 yenye kumbukumbu namba P/ZIU/M/02/09
kumshauri avunje mkataba wa mkandarasi huyo na kutangaza zabuni upya ya ujenzi
wa mradi wa Sangamabuni, jambo ambalo hadi leo hii halijafanyika na ndio maana
kumekuwa na malalamiko ya hapa na pale na mivutano isiyo ya lazima kati ya
halmashauri hiyo na kanda ya umwagiliaji.
Katika barua hiyo nanukuu moja ya kipengele
kilichomtaka mkurugenzi huyo avunje mkataba kinasema, “Therefore by using clause 62.2 (a) of the public procurement manual
which says that contractor stops work for 28 days when no stoppageof work is
shown on the current work program and the stoppage has not been authorized by
the project Manager, then this should be treated as a fundamental breach of the
contract. I advise you as a client to terminate the work and also to be
advertise again”.
Mkurugenzi wa
kampuni ya GS aliyejitambulisha kwa jina la Stephan Gamba ambapo alikiri
kutofanya kazi hiyo ya ujenzi kwa wakati, katika mradi huo wa umwagiliaji
Sangamabuni na kusema yeye amesogeza mawe tu katika eneo la mradi na taratibu
zingine za ujenzi zinafuata.
“Mwandishi ni kweli mradi huu sisi ndiye tuliyeshinda
zabuni, lakini ujenzi huu unakwamishwa na viongozi wenyewe sisi hatujashindwa
kuujenga”, alisema Gamba.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Shaibu
Nnunduma, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo hakupatikana na hata alipopigiwa
simu ili aweze kuzungumzia hilo alisema, yeye hawezi kutolea maelezo juu ya
miradi ya umwagiliaji ya wilaya hiyo kwa njia simu, na baadaye alikata simu.
Pamoja na mambo mengine leo naweza kusema utekelezaji
wa miradi mingi ya umwagiliaji kilimo cha mpunga wilayani hapa, haijalenga
matakwa yaliyowekwa na serikali licha ya kuwekeza fedha nyingi katika miradi
hiyo na ndio maana inajengwa kwa viwango visivyokubalika, kitendo ambacho
kimekuwa kikizua malalamiko mara kwa mara kutoka kwa wananchi.
Kwa ujumla ujenzi wa miradi ya umwagiliaji wilayani
Mbinga inakwama kutokana na viongozi husika kutowajibika ipasavyo juu ya suala
zima la kilimo kwanza.
Nimepita vijijini katika baadhi ya miradi ambako
inatekelezwa, malalamiko lukuki yamekuwa yakitolewa na wakulima wakidai kuwa
ujenzi mbovu wa mabanio na mifereji ya kupeleka maji mashambani ndio kikwazo
kikubwa kinachosababisha washindwe kutimiza adhma yao ya mapinduzi ya kijani.
Nakumbuka serikali hapa nchini iliitengea fedha
halmashauri ya wilaya hiyo shilingi bilioni 1.5 mwaka 2005 za ujenzi wa miundo
mbinu ya miradi hiyo ya umwagiliaji, lakini matokeo yake ya uzalishaji wa mazao
ni hafifu kitendo ambacho kinazua maswali mengi miongoni mwa jamii na bado
serikali imekuwa ikitoa fedha kila mwaka kwa ajili ya kuendeleza miradi hiyo.
Nashauri kuwa ni vyema serikali kupitia wizara yake ya
kilimo chakula na ushirika ikalifanyia kazi hili mapema ili kuondoa malalamiko
yaliyopo sasa hapa wilayani, kutoka kwa vikundi vya wakulima ambavyo vimeundwa
na vipo tayari kuzalisha zao la mpunga kwa njia ya umwagiliaji.
Ili tuweze kufikia malengo ya kauli mbiu ya kilimo kwanza
hapa nchini, sina budi kusema kuwa
watendaji ambao ni wazembe katika kusimamia suala zima la kilimo hicho ni vyema
wawajibishwe, ili iwe fundisho kwa watu wengine ambao ni wazembe katika
kusimamia maendeleo ya wananchi.
Siku zote watu wa Mbinga wengi wao ni wachapa kazi hususani
katika nyanja ya kilimo, na wanachohitaji ni usimamizi tu kwa kuelekezwa mbinu
bora za kilimo ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ninakumbuka mnamo mwezi
Oktoba mwaka jana aliitisha mkutano hapa nchini, uliowahusisha viongozi husika
na kuwapa maagizo ya kilimo yaliyofikiwa katika mkutano huo kuweka malengo ya
kuinua kilimo katika mikoa sita ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Ruvuma,
Kigoma na Rukwa.
Ili tuweze kufikia malengo yaliyofikiwa katika kikao
hicho ni vyema sasa viongozi katika mikoa hiyo hususani hapa wilayani Mbinga,
tusimamie ipasavyo fedha zinazotolewa na serikali ili tuweze kufikia malengo
yaliyokusudiwa na miradi ya umwagiliaji ijengwe kwa kufuata taratibu husika,
sio kuishia kulumbana kila kukicha na kusababisha maendeleo ya wananchi
kushindwa kusonga mbele.
No comments:
Post a Comment