Na Steven Augustino,
Tunduru.
JUMLA ya kesi 1064 zinazowahusu wazazi na walezi
walioshindwa kupeleka watoto wao shule, zimepangwa kuanza kusikilizwa ikiwa ni
juhudi ya serikali kuhakikisha kuwa watoto wote waliochaguliwa kujiunga na
masomo ya Sekondari, wanapelekwa shule.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho, alisema hayo
huku akifafanua kuwa, kesi zote zimepangwa kufanyika katika vijiji husika vya
wilaya hiyo.
Nalicho alisema hali hiyo imetokana na wazazi hao
kuendelea kukaidi maelekezo ya kupeleka watoto wao shule, hali iliyoisukuma serikali kumtafuta
hakimu, ambaye atahamishia shughuli za mahakama vijijini, ili kurahisisha kazi
za utekelezaji wa sheria.
Alisema wilaya yake ina shule 23 za Sekondari jumla ya
watoto 2764 walipangiwa kusoma katika shule hizo, lakini cha kushangaza hadi
sasa ni wanafunzi 1710 tu ndio walioripoti na kuanza masomo, ikiwa ni sawa na
asilimia 63 ya wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na masomo mwaka huu.
Pamoja na msimamo huo wa serikali wa kuwashitaki na
kuwachukulia hatua hizo za kisheria, mzazi atakayebainika kutompeleka mtoto
wake shule kwa makusudi atahukumiwa kifungo cha miezi sita jela, kutozwa faini
ya Tsh.300,000 au vyote kwa pamoja.
Mkuu huyo wa wilaya kufuatia hali hiyo amewaagiza maofisa
tarafa na watendaji wa vijiji kujiandaa kutoa ushahidi dhidi ya kesi walizozifungua,
kulingana na maelekezo ya ratiba ya kesi hizo pindi hakimu atakapotembelea na
kuendesha kesi hizo katika vijiji husika.
No comments:
Post a Comment