Friday, March 1, 2013

BWANA AFYA TUNDURU KUKIONA CHA MOTO


Na Steven Augustino,
Tunduru.

CHAMA cha Wanachi CUF kimetoa siku 14 kumtaka Bwana afya wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kutoa kibali cha kufungua Mbesa Hoteli iliyopo mjini humo, vinginevyo watafanya maandamano hadi katika ofisi za Mkuu wa wilaya hiyo kushinikiza hoteli hiyo ifunguliwe.

Tamko la kutaka kufanya maandamano hayo, lilitolewa katika mkutano wa kumkumbuka mwanzilishi na Mwalimu wa Siasa wilayani humo, marehemu Mazee Rajab aliyefariki Februari 17 mwaka 2010, uliofanyika katika viwanja vya Baraza la Idd mjini Tunduru.


Lengo la kumtaka mkuu huyo wa wilaya Chande Nalicho kufungua hoteli hiyo inatokana na kile kinachodaiwa kuwa, hoteli hiyo iliyopo katika mji huo imefungwa kwa njia ya uonevu.


“Kufungiwa kwa hoteli hii ni uonevu mtupu, sisi wananchi wa Tunduru tulikuwa tunapata chakula hapa kwa bei nafuu, sasa tunamuomba mkuu wa wilaya hii aliangalie hili ili haki iweze kupatikana”, walisema.


Wakifafanua tamko la malalamiko hayo kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa sheria na katiba wa chama hicho cha wananchi wilaya ya Tunduru, Jafari Majirani  na Durla Matala waliwatuhumu viongozi wa idara ya afya
wilayani humo, kuwa hufanya kazi zao kwa uonevu na hushiriki katika vitendo vya kuchukua rushwa.

Walisema hoteli hiyo ambayo hutoa huduma za chakula kwa bei nafuu imekuwa ni msaada mkubwa kwa watu wenye kipato cha chini, ikilinganishwa na hoteli ambazo hutoa huduma hiyo kwa bei za juu ambazo wao walidai hawana uwezo wa kumudu.  


Kuhusu sababu zilizotolewa na mabwana afya hao kuwa hoteli hiyo ni chafu na imekuwa ikitiririsha maji machafu hadi katika mifereji ya barabara kuu, walisema kuwa sababu hizo hazina msingi wowote kwani mifereji yote na mji mzima ni mchafu na wakawataka waanze kusafisha kwanza maeneo ya mji huo ya Tunduru ambayo mengi ni machafu.

Aidha viongozi hao pia wakatolea mfano wa uchafu katika maeneo wanayofanyia biashara za chakula kama vile mama lishe kuwa ni machafu zaidi, ikilinganishwa na mazingira ya hoteli hiyo kwamba ufungaji wake unaonesha kuwa na hila ama walilenga kumtishia mmiliki wake ili awapatie rushwa ndipo wamruhusu kufanya biashara hiyo.       



No comments: