Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
TANZANIA ni nchi ambayo
imejaliwa rasilimali nyingi ambazo zikitumika kwa ufasaha, taifa hili wananchi
wake kwa asilimia kubwa wanaweza kuondokana na umasikini ambao umekuwa ukiitesa
jamii nyingi miongoni mwao.
Lakini
inashangaza kuona licha ya kuwa na rasilimali hizo kama
vile madini ya aina mbalimbali, bado wananchi wake wamekuwa wakilalamika kila
kukicha kadiri siku zinavyozidi kwenda mbele.
Malalamiko
hayo yamekuwa yakielekezwa hasa kwa viongozi wa serikali ambao ndio wamepewa
dhamana na kusimamia misingi na taratibu nzuri ambazo zitamfanya Mtanzania
aweze kunufaika nazo.
Chakusikitisha
baadhi ya viongozi wetu ambao ndio wamepewa jukumu hilo, wanaonekana kutozingatia taratibu
husika, na kusababisha kelele na hata maandamano yasiyokuwa ya lazima ambayo
yanafanywa na wananchi wa eneo fulani ambako kero husika inatokea, yakilenga
kudai haki zao.
Katika
makala haya napenda kuelezea juu ya mgogoro uliojitokeza wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo wananchi wa kijiji cha
Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani humo Januari 29 mwaka huu, walitaka
kuandamana kwa masaa kadhaa kupinga kusafirishwa kwa makaa ya mawe ambayo
yanachimbwa kijijini humo, wakidai watekelezewe kwanza madai yao ya msingi ambayo mwekezaji husika anaonekana
kutoyatimiza.
Maandamano
ya mtindo huu ya wananchi kudai madai yao ya
msingi ni tatizo ambalo sasa nimeshuhudia limekuwa likijitokeza mara kwa mara
hapa nchini, ambapo hata mgogoro wa kupinga kusafirishwa kwa gesi kutoka Mtwara
hadi Dar es salaam
hali imekuwa bado ni tete hadi leo hii.
Makundi
yenye misimamo mikali yamekuwa yakiandamana huko Mtwara na kuitaka serikali itimize
ahadi zake ambazo ilizitoa kwa wananchi wale, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha
kusafisha gesi kabla haijasafirishwa, ujenzi wa
miundombinu ya barabara, umeme, kuimarishwa kwa bandari, mikopo kwa
wajasiriamali na viwanda vidogo vidogo vya ubanguaji wa korosho lakini
havijatekelezwa na ndio maana vinazua gumzo na maandamano yasiyokuwa ya lazima.
Lakini
tatizo hili limehamia hapa Mbinga na linatokana na wakazi hao kudai nyongeza ya
fidia zao katika eneo ambalo walihamishwa, kwa ajili ya kupisha kazi ya
uchimbaji wa makaa hayo na kupinga juu ya uchafuzi wa mazingira yakiwemo maji
katika mto Nyamabeva ambao unafanywa na wachimbaji wa madini hayo.
Maji ya mto huo yamekuwa yakitumika na wananchi hao
kwa shughuli mbalimbali majumbani mwao, lakini hivi sasa wanashindwa kuyatumia
kutokana na wachimbaji wa makaa hayo kutiririsha maji yenye mkaa wa mawe kuelekea
kwenye mto huo, na kusababisha baadhi ya viumbe kama
vile samaki kupoteza maisha.
Wakati hilo linatokea serikali wilayani Mbinga licha
ya kutuma wataalamu wake wa mazingira kwenda huko na kufanya upembuzi yakinifu
juu ya tatizo hilo, bado majibu hayajatolewa hadi leo hii kwa wananchi
wanaoishi jirani na makaa hayo juu ya athari za maji yenye kuchanganyika na
madini hayo yanavyoweza kuathiri afya zao, ambayo baadhi yao huendelea
kuyatumia na ndio maana walitaka kuandamana kudai haki yao.
Uongozi wa wilaya hiyo ukiongozwa na kamati ya ulinzi
na usalama, umeenda kule na kutumia mbinu za kuwatuliza tu wananchi wale na
kutoa kauli kwamba madai yao
yapo kwenye ngazi husika yanashughulikiwa, baada ya kuonekana hali ya kutaka
kuhatarisha amani kati ya kampuni inayochimba mkaa huo, Tancoal Energy katika
mgodi wa Ngaka, uliopo kijijini humo na wananchi hao kwa ujumla.
Pia jukumu lililochukuliwa na kamati hiyo kwenda huko
na kuamuru wachimbaji hao kuzuia maji hayo yenye mchanganyiko na makaa ya mawe
yasielekezwe katika mto huo ili kunusuru maisha ya wakazi hao.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya
umebaini kwamba vumbi kali la mkaa wa mawe limekuwa likienea katika vijiji
vilivyokuwa jirani na mgodi huo pale unaposafirishwa kwenda bandari ya Ndumbi
iliyopo katika ziwa Nyasa, Kiwira mkoani Mbeya na kiwanda cha kuzalisha saruji Tanga
kilichopo mkoani Tanga, huenda hali ya kiafya kwa wananchi wale ikawa hatarini
endapo hatua husika hazitachukuliwa kwa uharaka.
Nimezungumza na baadhi ya wananchi wa kijiji cha
Ntunduaro ambao hawakutaka majina yao
yatajwe gazetini, wakidai kwamba wamechoshwa na ahadi ambazo hazizai matunda na
utekelezaji wake unaonesha ukifanywa taratibu.
Wanasema madai yao wanahitaji majibu yatolewe haraka
juu ya uchafuzi wa maji ya mto Nyamabeva, ambao maji yake baada ya kuchafuliwa
na mkaa wa mawe wataalamu wa mazingira kutoka wilayani humo walikwenda na
kuchukua kiasi kidogo kwa ajili ya kuyafanyia uchunguzi wa kina, ili waweze
kubaini madhara yake na kwamba hadi sasa ni muda mrefu umepita hakuna majibu
yaliyotolewa.
Ofisa mtendaji wa kata ya Ruanda Matilda Nchimbi anasema
mgogoro huo wa wakazi kijiji cha Ntunduaro, unatokana pia na kampuni hiyo ya
Tancoal Energy kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya ukarabati wa
zahanati ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji na shule, jambo ambalo
limekuwa likizua malalamiko yasiyo na msingi badala yake wamemtaka mwekezaji
huyo atimize mambo ya msingi ili kumaliza malumbano hayo.
Wengine wametishia endapo hali hii itaendelea kudumu huenda
sasa kukatokea vurugu kubwa kama zile za
Mtwara, wakidai wamechoshwa na “longolongo” nyingi ambazo hazina manufaa kwao.
Wakati hilo likiendelea kufukuta, tafiti kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza
kwamba katika eneo hilo la mgodi wa makaa ya mawe kampuni hiyo ya Tancoal Energy
inamilikiwa kwa ubia kati ya serikali ya Tanzania na mwekezaji wa kampuni ya
Intra Energy, wameanza kuchimba kisima cha kwanza cha utafiti wa kuzalisha gesi
ya makaa ya mawe hapa nchini, katika mradi huo wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo
wilayani Mbinga.
Kisima hicho kinachimbwa katika eneo la Mbuyula kijiji
hicho cha Ntunduaro na ni miongoni mwa visima vitano vitakavyochimbwa na
Tancoal Energy katika mradi huo wa makaa ya mawe wa Ngaka.
Intra
Energy ambao ndio wabia wanamiliki asilimia 70
ya hisa za kampuni ya Tancoal Energy, kila kisima kitakachochimbwa
katika eneo hilo kitaweza kuzalisha megawati moja ya umeme, na huenda
hapo eneo hilo
litazalisha megawati tano kwa siku za hivi karibuni baada ya kukamilisha
ujenzi
wa mitambo hiyo ya kufua nishati umeme.
Kisima hicho cha kwanza hapa nchini, kuzalisha gesi ya
makaa ya mawe, gesi hiyo hupatikana mita zaidi ya 500 kwenda chini ya ardhi
ambayo inaitwa Coal Bed Methane.
Wakati uchimbaji huo wa kwanza wa kisima cha gesi ya
makaa ya mawe ukiendelea, kampuni ya Tancoal Energy ambayo ipo katika mchakato
wa kuanza kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ifikapo mwaka 2015, imetangaza
kuongeza kiasi cha kwanza cha umeme utakaozalishwa katika mradi wake wa Ngaka
kwa kufikia megawati 240 badala ya megawati 120 zilizotangazwa awali.
Ongezeko hilo linatokana
na kuongezeka kwa mashapo ya mkaa wa mawe ardhini katika eneo hilo, kulingana na matokeo ya utafiti
uliofanywa ambapo imethibitika kuwa eneo la Ngaka wilayani Mbinga, lina mashapo
mengi ya makaa yanayofikia tani milioni 356.
Endapo hilo
litatimia manufaa kwa nchi yetu ni kwamba kutoagiza tena makaa ya mawe kutoka
nje ya nchi, na kwamba viwanda vya saruji vilivyokuwa vikinunua makaa ya mawe
kwa dola 250 kwa tani, sasa vinapata makaa hayo kwa nusu ya bei hiyo tena mkaa
wenye ubora zaidi.
Wakazi wa kijiji cha Ntunduaro walionesha hofu ya
kutotimia hilo
kwa wakati kutokana na ubabaishaji wanaofanyiwa sasa wa hata kutolipwa fidia
zao kwa wakati, huku wakitoa shutuma nzito dhidi ya shirika la TANESCO nchini
kwamba ndio chanzo cha matatizo ya upatikanaji umeme.
Wamesema kwamba serikali endapo itatilia mkazo, shirika
hilo linaweza kuondokana na umeme wa dharula linaohangaika nao hivi sasa,
endapo litaamua kwa dhati kujikita katika uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe
katika mgodi huo wa Ngaka hapa wilayani Mbinga na kuunganisha kwenye mtandao wa
gridi ya Taifa.
Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya
ubia ya Tancoal Energy ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali,
kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa
na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.
Nionavyo kukalia kimya malalamiko ya wananchi ndipo
ulipo msingi wa matatizo mengi ya nchi hii, kila mtu anapenda na kutaka
kusifiwa lakini hakuna anayetaka kupokea lawama au hata wajibu wa kuwajibika
wengine wakifanya mabaya kwa niaba yao.
Hii leo sio Tanzania ile ya wanyonge ambao wanataka
ukombozi wa kweli katika mambo yanayohusu maisha yao na hawana muda wa
kusikiliza hadithi za kulindana na kupuuza malalamiko ya wananchi kama vile
tunavyoona sasa ulegevu katika kuchukua hatua dhidi ya wanaohusika na
malalamiko haya ya makaa yam awe Mbinga na hata ile gesi yetu ya Mtwara.
Kuendelea kwa matukio ya wananchi kuandamana kudai
haki zao za msingi, kunaonesha serikali yetu kutochukua hatua za haraka pale
wananchi wanapowasilisha matatizo yao
ya msingi hivyo yatupasa tubadilike tutekeleze mambo kwa vitendo na uhalisia
uonekane sio kupiga porojo.
No comments:
Post a Comment