Monday, March 25, 2013

MALI ZA USHIRIKA MBICU UTATA MTUPU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga. 

KAMA serikali mkoani Ruvuma, haitachukua hatua za haraka katika kusimamia na kukabidhi kwa njia halali mali za chama cha ushirika MBICU kilichopo wilayani Mbinga mkoani hapa, hakika huenda wanachama wenye mali hizo wasinufaike nazo.

Kumekuwa na mgogoro mzito unaoendelea kufukuta hapa wilayani, kutokana na viongozi husika kudaiwa kukabidhi mali za ushirika huo kwa njia za siri, bila wanachama ambao ni wakulima wa ushirika huo kupewa taarifa kamili juu ya hatma ya mali zao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kwamba, MBICU ni chama cha ushirika kinachojumuisha wakulima wanaozalisha zao la kahawa wilayani Mbinga.


Hivyo ushirika huo ambao ulikuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima hao, ulifikia hatua ya kufilisiwa mali zake mwaka 1998 kutokana na kudaiwa na serikali shilingi bilioni 1.1 na mali husika kuwa chini ya mufilisi.

Mali ambazo zilishikiliwa kutokana na kudaiwa deni hilo ni shamba la ugano lenye ukubwa wa ekari 1032, msitu wa kitelea, mradi wa maji(tanki la maji), viwanja kumi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za wafanyakazi ambavyo vipo jirani na tenki hilo, nyumba moja ambayo ipo katika mtaa wa Bwalo la mgambo Mbinga mjini, Mbicu hoteli ambayo ina eneo la ekari nane, ghala la pembejeo na kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga(MCCCO).

Serikali kwa huruma yake baada ya kuona ushirika huo unadaiwa deni hilo ulichukua jukumu la kufuta deni, na kuamuru mali zote za MBICU ambazo zilikuwa chini ya mufilisi wakulima wa ushirika huo warejeshewe mali zao mara moja, bila kuchelewa kwa kufuata taratibu husika.

Wakati hilo linafanyika tayari wakulima wa kahawa Mbinga walikwisha unda ushirika mwingine, unaojulikana kwa jina la MBIFACU ambao nao upo hadi sasa ukihusika katika kutetea maslahi ya wakulima wanaozalisha zao hilo wilayani hapa.

Kutokana na ukimya wa viongozi uliopo hapa mkoani Ruvuma, huenda hujuma zikafanyika kufuatia mali hizo kukabidhiwa kwa njia ya siri na wakati mwingine nusunusu, bila wanachama kujulishwa kupitia mkutano halali ambao ulipaswa kufanyika.

Mali hizo ambazo zinalalamikiwa ni kutokana, kutokabidhiwa bila wanachama husika kujulishwa ni kiasi gani cha mali zimekabidhiwa, ofisi ya vyama vya ushirika mkoa wa Ruvuma ndiyo iliyofanya makabidhiano hayo kwa bodi ya MBIFACU mnamo Oktoba 27 mwaka jana mjini hapa.

Watson Nganiwa ambaye ni ofisa msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani humo imeelezwa kuwa yeye na timu yake ndiyo ilifanya kazi hiyo, hivyo alipotafutwa kwa njia ya simu ili aweze kuzungumzia hilo simu yake ilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

Wakulima wengi ambao ni wanachama wamekuwa wakihoji kwa nini yafanyike makabidhiano ya siri, hivyo wamefikia hatua ya kutokuwa na imani na uongozi wa ushirika mkoa pamoja na bodi ya MBIFACU.

Wengi wao wamebaki kwenye sintofahamu na kufikia hatua chama cha wazee wastaafu wilayani Mbinga(OROAMBI) ambao husimamia na kutetea haki za masuala mbalimbali, wameingilia kati mgogoro huu na kulifikisha jambo hili katika ngazi husika.

OROAMBI ilimwandikia barua Mkuu wa wilaya ya Mbinga ambayo nakala yake tunayo, ya tarehe 10 Oktoba mwaka jana yenye kumbukumbu namba REF.ORO/11386/38 ikikataa kukabidhiwa mali za MBICU kwa njia zisizo halali.

Pia barua hiyo ililenga kumuomba Mkuu huyo wa wilaya ahakikishe makusanyo ya fedha, yanayoendelea kufanyika na mrajisi husika kwa mali za MBICU kuanzia mwaka 1999 hadi leo hii yakome, mpaka MBIFACU itakapokabidhiwa kwa taratibu halali mali zake.

Wametaka makusanyo hayo yaliyofanyika kwa kipindi cha miaka 13 huko nyuma hadi sasa yawekwe bayana, ambayo yanatokana na vyanzo vifuatavyo, kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga(MCCCO), Mbicu hoteli, ofisi za Mbicu na maghala yake, shamba la ugano na shamba la miti kitelea, tanki la maji lililochukuliwa na uongozi wa wilaya ya Mbinga bila kushirikisha wamiliki wa tanki hilo, viwanja na nyumba za kuishi wafanyakazi wa Mbicu.

Utafiti umebaini kuwa wateja wote wanaohodhi mali hizo za ushirika wa wakulima wa kahawa wilayani hapa, taarifa zake hazijawekwa wazi hivyo vigogo husika wanaendelea kuzikumbatia na ndio maana zinazua malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Licha ya Mkuu huyo wa wilaya kuandikiwa barua hiyo nakuombwa aliweke sawa jambo hilo, hali bado ni tete hakuna majibu yaliyotolewa kutoka katika ofisi yake hivyo OROAMBI iliamua kumuandikia barua mkuu wa mkoa wa Ruvuma, nakala yake tunayo ya tarehe 28 Januari mwaka huu yenye kumbukumbu namba ORO/11386/51 kumuomba kuingilia kati suala hili ili kutoa ushauri kwa wahusika na chama kikuu cha MBIFACU na vyama vingine vidogo vidogo vya ushirika(AMCOS) ambazo ni wanachama wa chama hicho kikuu, viweze kuimarishwa na kufanya biashara kama ilivyoainishwa katika katiba yake kifungu namba 1(5) g.

Kifungu hicho ambacho kinasema, na nukuu “To lease, purchase or operate mills, processing plants, storage accomodation, offices, transport and to provide such other services as shall from time to time be necessary to ensure the effective processing, marketing and distribution of its member societies produce”.

Wakati hilo likiendelea katika kipengele cha barua hiyo kimemweleza Mkuu wa mkoa kwamba kitendo cha kukaa kimya kwa Mkuu wa wilaya ya Mbinga, kamati ya OROAMBI inamtazamo hasi kwamba ni dalili ya kurudisha nyuma mafanikio ya Operate mills(mitambo) na marketing(biashara) kwa msimu wa mavuno ya zao la kahawa 2013/2014 hana sababu nayo yawezekana ana mtazamo wa mrengo wa kushoto katika kuiimarisha MBIFACU.

Vilevile barua ya Februari 18 mwaka huu yenye kumbukumbu namba ORO/11386/54 chama hicho cha wazee wastaafu wilayani Mbinga, kimemuomba Mkuu huyo wa mkoa kutuma wakaguzi waende wilayani humo, kukagua mauzo ya kahawa yaliyofanywa katika vyama vya ushirika vya Kimuli na Luwaita, kahawa hiyo ilikusanywa katika mchakato wa kulipa deni la kampuni ya Golden Impex ambayo ilihusika kukopesha pembejeo za kilimo kwa wakulima wa kahawa wilayani hapa.

Golden Impex ilikuwa inadai ushirika wa MBICU shilingi milioni 160 hivyo ikaona ili ijiridhishe makusanyo ya kahawa ya kulipia deni hilo na yafahamike, ni vyema Mkuu huyo wa mkoa atume timu yake ya ukaguzi na iwapo kutakuwa na salio lirejeshwe katika umoja wa wakulima wa MBIFACU.

Jitihada za mwandishi wa makala haya kumpata Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, aweze kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo hazikufanikiwa, hadi habari hizi zinaingia mitamboni.

Pamoja na mambo mengine sote tumekuwa tukitambua ushirika ndio msingi mkuu wa maendeleo ya mkulima, hivyo basi ni vyema sasa uongozi wa mkoa huo, ukasimama kidete ili kunusuru mali hizi za wakulima wa Mbinga zikabidhiwe kwa kufuata taratibu husika.

Kitendo cha kukabidhi mali kwa njia ya siri ni ishara tosha kuna jambo baya limetendeka na ndio maana leo wakulima wa kahawa wa wilaya hiyo, wamekuwa wakijia juu kutaka kujua na kupata hatma ya mali zao.

Jamii imekuwa ikitambua siku zote serikali, shughuli zake hufanya kwa uwazi na ukweli, iweje leo kiongozi wa ushirika wa mkoa wa Ruvuma anakabidhi mali kwa mtindo huo?

Nashauri mgogoro huu uliopo hapa Mbinga unapaswa kumalizwa mapema, kuendelea kulumbana kila siku ni kutomtendea haki mkulima huyu na tunahitaji tuambiwe bayana fedha za makusanyo ya MBICU tokea ifilisiwe ziko wapi, ili wakulima wanachokidai warejeshewe.


No comments: