Wednesday, March 27, 2013

AKINA MAMA TUNDURU WALIA NA HUDUMA ZA AFYA


Steven Augustino,
Tunduru.

SERIKALI imekumbushwa kutekeleza ahadi zake kwa vitendo, ili kuondoa kero ambazo zimekuwa zikilikabili kundi la wanawake na akina mama wajawazito, pale wanapohitaji kupatiwa huduma za matibabu na wakati wa kujifungua.

Hayo yalisemwa hivi karibuni na baadhi ya wanawake walioshiriki katika vikundi vya kwaya, ngoma, maigizo na ngonjera zilizofanyika wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika kiwilaya katika kijiji cha Mchoteka wilayani Tunduru hapa mkoani Ruvuma.


Wakifafanua taarifa hizo kupitia ujumbe uliotolewa kupitia nyimbo, wasanii  hao kutoka katika vikundi vya Njawanga na Kimamu walisema kuwa, mbali na viongozi hao wa serikali kuahidi utoaji wa huduma bure kwa wanawake wanaokwenda kujifungua katika vituo vya afya, zahanati na hospitalini bado hali ni tete kutokana na upatikanaji wa huduma hizo imekuwa kinyume huku kukiwa hakuna hatua zinazochukuliwa.

“sisi wanawake tuaotegemewa na taifa letu tumekuwa tukiteseka sana hasa wakati tunapokwenda kujifungua, kutokana na kunyanyapaliwa na waganga na wauguzi ambapo pamoja na kututaka kujigharimia wenyewe”, walisema.

Aidha wasaani hao wakaongeza kwa kuitaka serikali katika uboreshaji wa huduma hizo kwa wanawake wanaokwenda kujifungua, wagharimiwe na serikali yao ambayo waliiweka madarakani vifaa vyote muhimu, ili kuwaondolea kero na manyanyaso wanayoyapata sasa.

No comments: