Sunday, November 24, 2013

WAJASIRIAMALI WAMPA PONGEZI DIWANI WAO



Na Steven Augustino,
Tunduru.

KIKUNDI cha akina mama wajasiriamali wa tawi la Majengo B wilayani  Tunduru mkoa wa Ruvuma, kimempongeza Diwani wa kata ya Majengo  Athuman Nkinde kwa moyo wake wa kujitoa na kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali wilayani humo, ambayo aliahidi wakati wa kuwania nafasi hiyo mwaka
2010.

Mwenyekiti wa tawi la Majengo B la Chama cha Mapinduzi (CCM) Fatuma Mtesa alisema hayo wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa Mafunzo ya uzalishaji mali, kwa wanakikundi hao katika hafla fupi iliyofanyika viwanja vya ofisi za CCM katani humo.

Mtesa alisema kuwa katika mafunzo hayo ya siku 10 jumla ya akina mama wajasiriamali 46 walishiriki, ambapo yalitolewa chini ya ufadhili wa diwani Nkinde.

Tuesday, November 19, 2013

TUNDURU YAPONGEZWA KWA KUANZA UJENZI WA MAABARA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATIBU wa Siasa na ushirikiano wa kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dkt. Asha Rozi Migiro ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, kwa kuanza kwa kasi utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya maabara katika shule mbalimbali za sekondari wilayani humo, ikiwa ni juhudi ya serikali ya awamu ya nne kuinua taaluma kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi.

Dkt. Migiro ambaye amefuatana na Katibu mkuu wa CCM taifa   Abrahaman Kinana alisema hayo wakati alipokuwa katika shule ya sekondari ya kutwa, Mgomba sekondari iliyopo kata ya Majengo wilayani humo.

Alisema huo ni mpango ambao umewekwa na serikali katika kuhakikisha wilaya husika vyumba vya maabara vinajengwa katika shule ili kuinua kiwango cha taaluma katika masomo ya sayansi kwa wanafunzi.

Ujenzi huo unaenda sambamba na nyumba za walimu, nayo imekuwa ni kero kubwa hususani kwa shule zilizopo vijijini.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa maabara ya shule hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru Bw. Robart Nehatta, ambapo mkuu wa shule hiyo Elis Banda alimweleza Dkt. Migiro na msafara wake kuwa mradi wa ujenzi huo unatekelezwa kupitia  mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari(MMES II) katika mwaka wa fedha 2012/2013.   

Monday, November 18, 2013

WAANDISHI WA HABARI WANOLEWA MJINI DODOMA, WASISITIZWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI ZAO

Mratibu wa mafunzo ya kuandika habari na kuziweka kwenye mtandao Japhet Sanga (kushoto) kutoka TMF, akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ambao wanashiriki mafunzo hayo ya siku tano mjini Dodoma.

Mwandishi wa habari Franci's Godwin (aliyesimama) kutoka mkoani Iringa, akichangia hoja katika mafunzo ya siku tano ya uandishi bora wa habari na kuziweka kwenye mitandao, yanayoendelea kufanyika mjini Dodoma. (Picha zote na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Aliyekuwa Dodoma.

WAANDISHI wa habari nchini wamesisitizwa kuendelea kuzingatia misingi ya taaluma yao, ili kuweza kulinda heshima katika tasnia ya habari na taifa kwa ujumla.


Wito huo ulitolewa leo na Mratibu wa mafunzo ya habari za mitandao(Online Journalism) Japhet Sanga, kutoka shirika la Tanzania Media Fund (TMF) Jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na baadhi ya Waandishi wa habari mjini Dodoma.


Sanga alikuwa akizungumza na Waandishi hao, ambao wanashiriki mafunzo ya siku tano ya uandishi bora wa habari za uchunguzi na kuziweka mitandaoni, yanayofanyika kwenye ukumbi wa New Dodoma hotel uliopo mjini hapa.


Waandishi hao ni wale ambao wanashughulika katika majukumu ya kazi zao za kila siku, katika kuandika habari na kuziweka kwenye mitandao yao.


“We want to have Quality blogger's…………… tunahitaji mtu ambaye anazingatia maadili ya vyombo vya habari, hatuhitaji mtu anayeandika vitu vyenye kulenga uchochezi”, alisema.



Naye Mkufunzi mkuu wa mafunzo hayo Beda Msimbe alisema, katika zama hizi Waandishi wengi wamekuwa wakizembea kuzingatia maadili ya kazi zao, na hivyo kujikuta jamii kukosa imani nao.  

KATIBU MKUU WA CCM TAIFA AKUMBANA NA KERO YA KOROSHO TUNDURU, WATENDAJI WIZARA YA KILIMO WATILIWA SHAKA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa Abrahaman Kinana ambaye anaendelea na ziara yake wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amekutana na kero inayoendelea kulitesa Soko la korosho huku wananchi wa wilaya hiyo wakilalamikia kwamba tatizo hilo kutokana na kudumu kwa muda mrefu, linawafanya wakose imani na Wizara ya kilimo chakula na ushirika ambayo ilipaswa kusimamia.


Kufuatia hali hiyo Kinana naye ilimlazimu kutilia shaka utendaji wa Wizara hiyo na kuahidi kuwa litafanyiwa utekelezaji wa haraka ili kuondoa kero hiyo iliyopo sasa. 


Kilio hicho cha Wakulima wa korosho wilayani Tunduru kilijitokeza katika vijiji vya Lukumbo, Munjaku, Mchoteka, Nalasi na Mtina vilivyopo katika Jimbo la Tunduru Kusini wilayani humo.  

Wednesday, November 13, 2013

UHARIBIFU WA MAZINGIRA NA UCHOMAJI MOTO MISITU WATISHIA KUTOWEKA KWA VYANZO VYA MAJI RUVUMA

Mazingira yanavyoharibiwa kama hivi, ni hatari kwa maisha ya binadamu na viumbe hai. 

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WANANCHI waishio mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuwa na tabia ya kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji na kuvifanya kuwa endelevu, kwa  faida ya vizazi vijavyo na hata kwa matumizi yao wenyewe ili waweze kuwa na maisha endelevu.

Hivi sasa kumekuwa na kasi kubwa ya uharibifu wa vyanzo hivyo kunakosababishwa na shughuli za kibinadamu kama vile kilimo na ufugaji hali ambayo inatishia kutoweka kwa uoto wa asili.

Wito huo ulitolewa na mshindi wa tuzo ya mazingira ambaye pia ni mwanaharakati  wa msuala ya mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji mkoani Ruvuma, Menas Andoya alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea, kuhusiana na kasi  kubwa ya uchomaji  moto misitu na uchafuzi wa vyanzo vya maji ambao umeshamiri mkoani humo.

Alisema viongozi kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji   na hata kata wanapaswa kusimamia kikamilifu suala la utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji kutokana na wao ndiyo wanaoishi na wananchi.

WAZAZI WILAYANI TUNDURU WATAKIWA KUWAJENGEA WATOTO WAO MALEZI BORA

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WAZAZI na Walezi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameaswa kushirikiana na serikali kusimamia na kufuatilia   kwa karibu mienendo na maendeleo ya watoto wao hasa wa kike, ikiwa ni juhudi ya kuhakikisha  kuwa  watoto hao wanafanya  vizuri katika masomo yao na kujiletea maendeleo yao.

Ofisa mtendaji wa kata ya Mhuwesi  Shijabu Ngoronje alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa Wadau wa elimu uliofanyika katika Kijiji cha Mhuwesi, ukiwa ni mwendelezo wa juhudi za mradi  wa usimamizi na utetezi wa haki ya mtoto wa kike kupata elimu .

Akifafanua taarifa hiyo Ngoronje alisema, ili kufanikisha adhima hiyo serikali imejipanga kutoa elimu kwa kuwaomba wazazi na walezi kujitoa kuchangia chakula  cha mchana kama kivutio kwa watoto wao na kuwafanya wapende masomo.

Saturday, November 9, 2013

WALEMAVU WA MKOA WA RUVUMA WALIA NA SERIKALI, WASEMA UNYANYAPAA UMEKITHIRI KATIKA NYANJA MBALIMBALI

Mgeni rasmi Anton Nginga ambaye ni Afisa maendeleo ya jamii mkoani Ruvuma, akihutubia katika mkutano wa uchaguzi wa viongozi CHAWATA wa mkoa huo, kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Songea uliopo mjini hapa.


Baadhi ya Wajumbe ambao ni Watu wenye ulemavu, wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi(hayupo pichani) wakati alipokuwa akihutubia katika  mkutano wao.

Mwenyekiti wa CHAWATA Songea mjini, ambaye amesimama Kassim Mgwali akisisitiza jambo kwa kuitaka serikali, izingatie uwepo wa mahitaji muhimu kwa watu wenye ulemavu.           (Picha zote na Kassian Nyandindi)





Na Kassian Nyandindi,

Songea.

IMEBAINISHWA kuwa changamoto kubwa inayoathiri maendeleo ya watu wenye Ulemavu mkoani Ruvuma, ni unyanyapaa uliokithiri katika nyanja mbalimbali, ikiwemo mazingira magumu ya kupata elimu na kuwezeshwa kiuchumi kuweza kupata nafasi ya kuingia katika vyombo vya maamuzi.

Aidha uongozi wa halmashauri za mkoa huo umetupiwa lawama kwamba umekuwa ukiwatenga kundi la watu hao, pale wanapohitaji msaada au ufafanuzi wa mambo mbalimbali.

Kufuatia hali hiyo, serikali imeombwa kuingilia kati na kuhakikisha tatizo hilo linafanyiwa kazi ikiwemo ushirikishwaji kwa watu wenye ulemavu katika kupanga bajeti ya maendeleo kwa ngazi mbalimbali, uwe unatekelezwa ipasavyo.

Hayo yalibainishwa na Wajumbe wa mkutano Mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi ya mkoa wa Ruvuma, uliofanyika leo kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea uliopo mjini hapa na kuhudhuriwa na mgeni rasmi afisa maendeleo ya jamii wa mkoa huo, Anton Nginga.

Thursday, November 7, 2013

MADIWANI TUNDURU WALIA NA SEHEMU YA KUJIFUNGULIA AKINA MAMA WAJAWAZITO, WENGINE WAJIFUNGULIA SAKAFUNI

Na Steven Augustino,
Tunduru.

MADIWANI wa viti maalumu katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameomba kuridhia na kuruhusu kufunguliwa kwa wodi mpya iliyojengwa katika hospitali ya Wilaya hiyo kwa ajili ya kujifungulia akina Mama wajawazito, wanaoenda kupata huduma hiyo muhimu hospitalini hapo kwa kuanza. 


Kilio hicho kilianza kuwasilishwa na Diwani wa Viti maalumu wa Tarafa ya Matemanga Stawa Omari huku akiungwa mkono na Swema Kalipungu wa Tarafa ya Mlingoti na Alus Yunus wa Nalasi walisema hivi sasa hali ya akina mama hao ni tete kutokana na wengine hujifungua wakiwa wamelala chini sakafuni.
  

Madiwani hao walisema kuna wakati akina mama wajawazito wamekuwa wakijifungulia katika chumba cha kupokelewa wagonjwa. 


Walidai kuwa imefikia hatua wakati mwingine hata wagonjwa wanaoenda kupata matibabu hospitalini hapo hupata shida pale wanapohitaji huduma za vipimo choo ndogo na kubwa ambapo hulazimika kwenda vyoo vya nyumba za jirani kutokana na miundo mbinu ya hospitali hiyo kutotosheleza.


Walisema kila wanapohitaji maelezo kwa wataalamu husika wamekuwa wakiambiwa kuwa tatizo linalo wa kwaza ni kutokana na wodi hizo mpya kutokamilika miundo mbinu husika.

  
Aidha madiwani hao waliendelea kuiomba halmashauri kutenga eneo jingine la kujifungulia akina mama, ambao wanaenda kujifungua katika hospitali hiyo kujisitiri mahali pa zuri. 

Sunday, November 3, 2013

BARAZA LA MADIWANI WILAYANI MBINGA LAMSHUSHIA RUNGU AFISA ELIMU TAALUMA, WAMKATAA WATAKA AREJESHWE KWA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa.














Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.


HATIMAYE Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limefanya maamuzi mazito ya kumkataa Afisa Elimu Taaluma wa wilaya hiyo Rashid Pilly, na kumwagiza Mkurugenzi na Mwenyekiti wake wa halmashauri hiyo kumwondoa haraka afisa huyo na kumrejesha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi.


Pilly analalamikiwa kwa muda mrefu kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kikwazo katika utendaji kazi wa idara hiyo, amekuwa akitumia muda mwingi badala ya kufanya kazi husika, yeye amekuwa akiandika barua zenye kuzua migogoro, kuchafuana na kugombanisha wafanyakazi wenzake na afisa elimu wa wilaya hiyo Mathias Mkali.


Hatua ya Madiwani hao kumkataa Afisa elimu taaluma wa wilaya hiyo, imejitokeza hivi karibuni katika kikao cha Baraza hilo kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la Maendeleo, uliopo mjini hapa.


Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wilayani Mbinga ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho, Winfrid Kapinga alisema wamekasirishwa na tuhuma hizo na kubaini kwa muda mrefu kuwa vitendo hivyo vinavyofanywa na Pilly, vinaweza kudumaza mikakati iliyowekwa ya kimaendeleo katika kukuza elimu wilayani humo.


Kapinga alifafanua kuwa Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Bw. Mkali alipohamia wilayani Mbinga mwaka 2011 aliweza kuinua kiwango cha taaluma kutoka asilimia 40 hadi kufikia asilimia 53.6 na kuifanya halmashauri hiyo kushika nafasi ya pili mkoani Ruvuma, kati ya wilaya tano zilizopo mkoani humo.


“Tumeamua kumkataa huyu mtu kutokana na matendo yake, ni vyema arejeshwe kwenye mamlaka yake ya uteuzi ili kuondoa migogoro hii ambayo imekuwa kero kubwa katika idara hii ya elimu”, alisema Kapinga.


Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Mkali alipohamia wilayani Mbinga, aliweza kukabiliana na tatizo la watoto 1,744 wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK) kwa kuweka mikakati madhubuti ambayo ilishirikisha walimu wote mashuleni na kuifanya wilaya hiyo iweze kusonga mbele.


Pamoja na mambo mengine, Diwani wa kata ya Litembo Altho Hyera alipozungumza na Waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mikutano, alisema hatua iliyochukuliwa na baraza hilo inapaswa kuungwa mkono huku akieleza kuwa Pilly amekuwa akiendeleza migogoro ya kuandika barua hizo, kwa kushirikiana na Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) tawi la Mbinga Samwel Mhaiki na kuufanya uongozi wa wilaya hiyo kushindwa kufanya kazi zake za kimaendeleo, kutokana na muda mwingi kuutumia kujibu tuhuma wanazoziandika katika barua hizo na kuzipeleka ngazi ya juu.


“Huyu Pilly muda mwingi yeye badala ya kufanya kazi anafikiria kuandika mabarua ya kuchafuana yasiyo na faida kwetu, kamati husika iliundwa kufuatilia jambo hili na imebaini kuwa hakuna ukweli wa mambo anayo andika na sisi tumeona hatufai………..aondoke”, alisema Hyera.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya elimu, afya na maji wilayani Mbinga ambaye ni Diwani wa kata ya Litumbandyosi, James Yaparama alieleza kuwa wamechoshwa na mambo yaliyofanywa na  afisa elimu taaluma wa wilaya hiyo hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kukaa na mtu ambaye muda mwingi amekuwa akileta matatizo katika wilaya yao ambayo yakiendelea kufumbiwa macho huenda maendeleo katika sekta ya elimu yakarudi nyuma.


Hata hivyo alipoulizwa Pilly alieleza kuwa yeye tuhuma hizo anazisikia tu watu wakizungumza mitaani na bado hajapata barua rasmi ya kumuhamisha katika kituo chake cha kazi kutoka kwa mwajiri wake, huku akiongeza uamuzi uliochukuliwa na baraza hilo hautambui na ataendelea na kazi kama kawaida ambapo vilevile alipotafutwa kwa njia ya simu Katibu wa CWT tawi la Mbinga, Samwel Mhaiki ili aweze kujibia suala la kuhusishwa na tuhuma hizo, hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa imefungwa kwa muda mrefu.