WAZIRI wa Maendeleo ya
Mifugo na Uvuvi Dokta Titus Kamani, amesema ili kwenda na kasi ya maboresho ya
wizara hiyo, inahitajika dhana ya uwajibikaji na uwazi sambamba na kujitolea
kwa nguvu zote katika kufanya kazi.
Kamani, aliyasema hayo
juzi katika mkutano wa kwanza uliowakutanisha wafanyakazi wote wa wizara hiyo,
wakiwemo wastaafu wa mwaka jana katika ofisi ya wizara hiyo ilizopo Temeke
jijini Dar es Salaam.
Alisema kama kuna mtu ambaye ni
kikwazo katika kukwamisha shughuli za wizara, ni bora akawapisha mapema na
kwamba kila mtumishi kwa nafasi yake, anatakiwa kuifanya kazi kwa uwazi na
akaitaka wizara kufanya kazi na vyombo vya habari kwani ndio njia pekee ya
kuwafanya watanzania wajue wizara inafanya nini.
“Wewe upo ofisini, halafu
unaogopa ogopa vyombo vya habari, kwani unatatizo gani kuweni wazi mambo yenu
yawe hadharani watanzania wa Mbeya wayajue, Rufiji mpaka Pemba, hakuna kuficha
ficha jambo katika wizara yangu.” alisistiza Dokta Kamani.
Alisema wizara ya maendeleo ya
mifugo na uvuvi ndio moyo wa taifa kwani huwajumuisha watanzania wengi wenye
maisha ya kawaida, lakini amesikitishwa kwa jinsi ambavyo wizara hiyo imekuwa
ikichukuliwa na baadhi ya watu kama ni wizara yenye migogoro na kuleta hasara
maeneo mengine.