Saturday, July 11, 2015

AJINYONGA KUTOKANA NA KUDAIWA DENI

Na Mwandishi wetu,
Songea.

WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti, yaliyotokea wilayani Nyasa na Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, likiwemo la fundiseremala mmoja kujinyonga kutokana na kukimbia deni alilokuwa akidaiwa.

Akifafanua juu ya matukio hayo, Kamanda wa Polisi mkoani humo Mihayo Msikhela alisema tukio la kujinyonga lilitokea mtaa wa Ostarbey, katika kata ya Msamala Songea mjini.

Katika tukio hilo marehemu aliyefahamika kwa jina la PeterLufunda (38) alichukua hatua ya kujinyonga, baada ya Mahakama ya wilaya ya Songea kutoa hukumu ya kuiruhusu SACCOS ya mtaa huo kuuza nyumba yake aliyokuwa akiishi, ili kulipa deni la mkopo wa shilingi milioni 1 ambalo alikopa na kushindwa kulipa.


Msikhela alieleza kuwa, kwa mujibu wa maelezo ya ujumbe alioacha kwa familia yake kutoshitushwa na maamuzi hayo, bali wajitahidi kumuombea kwa mwenyezi Mungu na kumtunzia watoto wake.

Pamoja na mambo mengi, tukio la pili linahusisha wavuvi wawili ambao ni wakazi wa kijiji cha Mkalole katika eneo la mto Ruhekei, waliopoa mwili wa mtu anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 45 hadi 50 akiwa amekufa maji.


Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi aliongeza kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya hiyo, kwa ajili ya ndugu kwenda kuutambua kutokana na wavuvi hao kutomfahamu.

No comments: