Sunday, July 5, 2015

WAJAWAZITO WAJIFUNGULIA MWANGA WA TOCHI YA SIMU

Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, akihutubia wananchi wa kata ya Linga wilayani humo hivi karibuni.
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.

AKINA mama wajawazito wanaopatiwa matibabu katika kituo cha afya Litumba kuhamba kata ya Linga, wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wanapata shida wakati wa kujifungua nyakati za usiku, kutokana na kukosa nishati ya mwanga.

Kufuatia hali hiyo wauguzi wa kituo hicho cha afya, wanalazimika kutumia tochi za mwanga wa simu pale mama mjamzito, anapofikia hatua ya kutaka kujifungua.

Hayo yalisemwa na Muuguzi wa kituo hicho, Witness Mtende mbele ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani humo, Cassian Njowoka alipokuwa ametembelea kituo hicho kwa ajili ya kukabidhi msaada wa vifaa vya mfumo wa nishati ya umeme wa jua (Solar).

Mtende alisema pia wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maji, nyumba za kuishi wahudumu wa afya hivyo wanaiomba serikali, ifanye jitihada ya kumaliza kero hiyo.


Kwa upande wake Kamanda UVCCM wa wilaya hiyo, Njowoka baada ya kukabidhi msaada huo aliweza kutoa ahadi ya kufanya ukarabati wa chumba cha kujifungulia na kupumzikia akina mama wajawazito, kwa kuweka maru maru kutokana na vyumba hivyo kuwa chakavu.

Vilevile Kamanda huyo wa Umoja wa vijana alitoa vitanda 11 vya kulaza wagonjwa, magodoro yake na mito ya kulalia wagonjwa katika kituo hicho cha Litumba kuhamba, ikiwemo na kitanda kimoja cha kujifungulia akina mama wajawazito.

No comments: