Na Steven
Augustino,
Tunduru.
MFANYABIASHARA mmoja ambaye ni maarufu kwa kuuza viazi vitamu,
katika kitongoji cha Ng’apa kijiji cha Namiungo wilayani Tunduru mkoa wa
Ruvuma, Bibiye Yasin Mkao (43) amefariki dunia baada ya kugongwa na lori.
Chanzo cha ajali hiyo kimeelezwa kuwa kimetokana na dereva
aliyekuwa akiendesha gari lenye namba za usajili, T 442 CBM ambalo ni mali ya
kampuni ya kichina Synohdro, inayojenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka wilaya
ya Tunduru kwenda Mangaka mkoani Mtwara.
Diwani wa kata hiyo, Nurdin Mnolela alisema marehemu huyo
aligongwa na lori hilo la kichina aina ya Howo Syno truck ambalo lilikuwa
likiendeshwa na dereva, Noel Beda ambaye mpaka sasa ametokomea kusikojulikana.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema
kuwa wamejipanga kumsaka mtuhumiwa wa tukio hilo, kwa lengo la kumfikisha
Mahakamani ajibu tuhuma inayomkabili.
Dokta Joseph Ng’ombo ambaye aliufanyia uchunguzi mwili wa
marehemu Mkao, alisema kuwa chanzo cha kifo hicho kilitokana na kutokwa na damu
nyingi, baada ya kupasuka fuvu la kichwa.
Sambamba na hilo, marehemu alipata pia mivunjiko katika
maeneo mbalimbali ya mwili wake ikiwemo miguu, mikono na mbavu.
No comments:
Post a Comment