Sunday, July 19, 2015

KALOLO NA HARAKATI ZA KUPATA UBUNGE TUNDURU KASKAZINI

Ajili Kalolo, mgombea nafasi ya ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani Ruvuma, akionesha fomu ya kugombea mara baada ya kuichukua kutoka ofisi za CCM wilayani Tunduru.
Na Steven Augustino,
Tunduru.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Tunduru kaskazini wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini na kutokubali kutumiwa na wajanja wachache wanaopita kuwanadi wagombea wanaowania nafasi ya ubunge katika majimbo ya uchaguzi wilayani humo, ambao wakishapata nafasi hiyo huondoka na kwenda kuishi mbali na majimbo yao.
Aidha wanachama hao ambao ni wakereketwa wa CCM, pia wametahadharishwa dhidi ya wagombea wa nafasi hiyo ambao wamekuwa na tamaa ya madaraka, hivyo wameshauriwa kuwachuja kwa hoja zao majukwaani, ili kuona kama kweli watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia wananchi pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya kuwaongoza.
Hayo yalisemwa na kada wa Chama Cha Mapinduzi na afisa wa idara ya utawala na uwezeshaji  jumuiya ya wazazi  makao makuu ya chama hicho, Omary Kalolo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya chukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge katika jimbo hilo ambalo awali lilikuwa linaongozwa na mhandisi Ramo Makani.
Alisema kwamba licha ya kila mwanachama wa chama hicho, anayohaki ya kuchukua fomu na kuomba ridhaa ya kuingia katika kinyang’anyiro hicho, lakini wanapaswa kumchagua mtu makini na mwenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi wake na sio vinginevyo.

 “Ndugu zangu mwaka huu tuwe waangalifu sana, tuchague viongozi bora kwenye uchaguzi wa kura za maoni katika chama chetu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, tuwe waaminifu tusichague kiongozi ambaye baadaye tutashindwa kumuuza kwa wananchi wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika”, alisema Kalolo. 
Alisema katika mchakato huo yeye ndiyo chagua sahihi la wananchi wa jimbo hilo, na ni mzawa ambaye hawezi kuwaangusha katika uwakilishi wake bungeni.
Pamoja na mambo mengine, aliwataka kushikamana na kuhakikisha kwamba CCM kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Awali akizungumzia haki za mgombea baada ya kuchukua fomu hizo mbele ya kada huyo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilayani Tunduru, Mohammed Lawa alimtahadharisha kuwa kada huyo kuwa kwa sasa hataruhusiwa kufanya kampeni hadi taratibu zitakapokamilika ambapo chama hicho kitatembea na wagombea wote na kuwanadi kwa wanachama wake.

No comments: