Stanford Nyambo (Tinga tinga) |
Na Dustan Ndunguru,
MWAKA huu unatarajiwa
kufanyika uchaguzi mkuu ambapo Madiwani, Wabunge na Rais watachaguliwa na
kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, ambapo uchaguzi huo utafanyika kwa
kuvihusisha vyama ambavyo vimesajiliwa kisheria.
Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ndicho chama kinachoongoza nchi ya Tanzania kwa kipindi kirefu sasas, kwa
kuhakikisha amani na utulivu kwa wananchi wake vinaendelea kuwepo.
CCM ni chama ambacho Watanzania
wengi wanakiamini na kukichagua kushika dola tangu kuanzishwa kwa mfumo wa
vyama vingi mwaka 1992.
Watanzania hawa wameamua
kwa dhati kuwachagua wagombea waliotokana na chama hiki tawala, kutokana na
kuridhishwa na sera zake nzuri ambazo kimsingi zimekuwa zikilenga kuwaletea
maendeleo wananchi, ikilinganishwa na sera za vyama pinzani.
Udiwani ni moja kati ya
nafasi ambayo wanachama wa CCM, watakuwa na haki ya kuchagua au kuchaguliwa
kama katiba ya chama inavyosema ambapo wakati ukifika kura za maoni ndani ya
chama zitafanyika na kupatikana wagombea ambao wataingia kwenye kinyang’anyiro
cha uchaguzi mkuu ambako pia wapinzani nao watasimamisha wagombea wake.
Kila chama cha siasa
kimejiwekea utaratibu wake wa kuwapata wagombea, ambao watasimama siku hiyo
ambayo utafanyika uchaguzi mkuu huku wananchi wakiwa na wajibu wa kuwapigia
kura wale ambao wanaimani nao kwamba, wakishinda watashirikiana nao vyema katika
kujiletea maendeleo.
Chama cha mapinduzi, kinao
utaratibu wake ambao kimejiwekea ikiwa ni njia ya kuwapata wagombea wake
watakaosimama kwa niaba ya chama, ili wapigiwe kura na wananchi.
Utaratibu uliowazi kwa sasa
ni ule wa upigaji kura za maoni, wanachama wa chama hicho watawapigia wagombea
watakaojitokeza kuomba nafasi za udiwani, ubunge na urais ambapo kwa wale ambao
watasimamishwa na chama wataweza kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo.
Majimbo na kata mbalimbali
za uchaguzi hapa nchini, wanachama wa chama hiki tawala wamekuwa wakijitokeza
na kutangaza nia yao ya kugombea kwa nafasi hizo, ambapo watachujwa katika kura
za maoni ndani ya chama kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.
Kata ya Mtipwili iliyopo
mkoani Ruvuma, ni moja kati ya kata ambayo wanachama wa chama hicho
wamejitokeza na kutangaza nia ya kugombea kwa nafasi hiyo ya udiwani, ambapo
kata hivi sasa inajumuisha vijiji vya Matenje, Mtipwili, Chiulu na Malini.
Stanford Nyambo kwa jina
maarufu Tingatinga, ni mmoja kati ya wanachama wa chama cha mapinduzi ambaye
ametangaza nia yake ya kugombea nafasi hiyo na kuelezea mikakati yake atakayoitekeleza endapo kama
wananchi wa jimbo hilo watampatia ridhaa ya kuwaongoza.
Nyambo anasema kimsingi
wananchi wake wamekuwa wakijihusisha na shughuli za uvuvi, kilimo cha kahawa ikiwa
ni njia kuu ya uchumi pamoja na uchimbaji mdogo wa madini huku wengine wakijishughulisha,
na uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula.
Kupitia uvuvi na kilimo anasema
atahakikisha anatafuta zana za kisasa za kufanyia shughuli zao, kwa lengo la
kuimarisha shughuli za uvuvi kwa wavuvi, ili waweze kupata mapato makubwa na hatimaye
wajikwamue kiuchumi.
Anasema anaamini kwamba
kama atachaguliwa kuwa mwakilishi wao atashirikiana na wakulima, kuzalisha
mazao bora ya chakula na biashara ambayo yatapata bei nzuri sokoni.
Kwa upande wa kilimo
atahakikisha uzalishaji wa korosho na mazao mengine kama vile ufuta na mpunga,
vinapewa kipaumbele kutokana na ukweli kwamba mazao hayo hustawi vizuri katika
kata ya Mtipwili.
Kuhusu masoko ya mazao yatokanayo
na uvuvi, kilimo anaelezea kuwa atahamasisha uundaji wa vikundi vya
ujasiriamali, ambavyo wataalamu wa kilimo wataweza kuwafikia wanachama husika
kwa urahisi na kuwapa elimu ya uzalishaji bora wa mazao yao.
Anasema kauli mbiu yake ya
“Pambazuko jipya la maendeleo” katika kata ya Mtipwili itasaidia kufikia
mafanikio wanayotarajia kuyapata wananchi na kwamba amedhamiria kuisimamia kwa
dhati kauli mbiu hiyo, katika kipindi chote cha utawala wake kama atapewa
ridhaa na wananchi kuwaongoza.
Anafafanua kuwa zipo
changamoto mbalimbali, ambazo wazalishaji wa mazao wanakabiliana nazo hivyo yeye
binafsi atahakikisha anashirikiana nao kikamilifu, katika kuzikabili changamoto
hizo.
Kuhusu mazao mengine
anasema kuwa atahamasisha wakulima wazingatie maelekezo ya wataalamu husika, ili
waweze kuzalisha kwa wingi hasa ikizingatiwa yapo mazao kama vile mahindi, ulezi,
matunda na mengineyo yanastawi vizuri katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Nyambo anazungumzia pia
sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara kwamba atashirikiana na serikali
na wananchi kwa ujumla, ikiwa ni lengo la
kuboresha sekta hizo muhimu.
Anasema miundombinu katika
baadhi ya maeneo ya kata hiyo ni mibovu, jambo ambalo wananchi hupata shida hasa
nyakati za masika wakati wa kusafirisha mazao yao na hata huwawia vigumu
kuwafikisha wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Nyasa pale wanapotakiwa
kupatiwa matibabu.
Anasema atahakikisha kila
eneo katika kata, linafikika kwa urahisi kwa kuondoa vikwazo vyote akihakikisha
serikali inajenga madaraja ya kudumu na vivuko vya uhakika ambavyo vinapitika
wakati wote.
Iwapo kama atapata ridhaa
ya wananchi kuwaongoza kata hiyo, atakuwa na vikao vya mara kwa mara
na wananchi kabla na baada ya vikao vya baraza la madiwani, ili
kupata maoni ya wapiga kura wake na kuimarisha umoja na upendo.
Tingatinga anabainisha kuwa
kata ya Mtipwili ina fursa nzuri ya kuharakisha maendeleo na uchumi kwa ujumla
hasa ikizingatiwa kata hiyo ina mazingira mazuri, ambayo kama yatafanyiwa kazi
ipasavyo vipato vya wananchi vitaongezeka.
Anasema wananchi
wanalojukumu kubwa la kubadilisha mtazamo wao ili waweze kufikia kiu ya
maendeleo waliyonayo sasa na kuondokana na umaskini jambo ambalo linahitaji
kiongozi makini, ambaye ana uchungu wa dhati juu ya wananchi wa kata yake.
Tingatinga anasema
kuwa kinachotakiwa sasa kwa wanachama wa chama cha mapinduzi, kuhakikisha wanakuwa
makini kuwachagua viongozi ambao watawapa maendeleo ya kweli na wajihadhari na
wagombea ambao wanamawazo mgando ikiwemo hutumia fedha kununua uongozi.
Anasema kuwachagua wagombea
kwa sababu ya fedha walizonazo huku uwezo wa kuongoza ni mdogo, haina maana
kwani mwisho wa siku watajikuta mwakilishi wao akijilimbikizia mali.
Kuhusu chama cha mapinduzi
anasema yeye anatambua wazi kuwa ni mwanachama halali wa CCM, hivyo kama
atachaguliwa kuwa mbunge atahakikisha anarejesha matunda kwa chama chake ambapo
kwa kushirikiana na wanachama kila tawi litakuwa na ofisi yake ya tawi na
kuongeza idadi ya wanachama.
Tingatinga ambaye pia ni
katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya ya Nyasa anasema pamoja na wadhifa huo
pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa tawi la Mtipwili, wa CCM wa kata hiyo na wa
baraza la migogoro la kata ambapo katika kipindi chake cha uongozi wa chama alihimiza
pia kufungua matawi ya Mtulima, Likalo B, Tembwe na Mtulivu wilayani Nyasa.
No comments:
Post a Comment