Mwandishi wa habari Kassian Nyandindi, ambaye ametangaza nia ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi. (CCM) |
Na Dustan
Ndunguru,
Mbinga.
KASSIAN Nyandindi ambaye amebobea katika fani ya uandishi wa
habari, na sasa anaandikia gazeti la Majira mkoani Ruvuma, ametangaza nia yake
ya kugombea udiwani katika kata ya Mbinga mjini A, iliyopo wilayani Mbinga
mkoani humo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza leo na vyombo mbalimbali vya habari mjini hapa, Nyandindi
alisema amekwisha chukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na kuirejesha, huku akitamka vipaumbele vyake endapo wananchi wa kata hiyo watampatia ridhaa
ya kuwaongoza, atahakikisha huduma muhimu za kijamii zinaboreshwa.
Alisema atazingatia kwamba miundombinu mbalimbali kama vile
barabara za mitaa, afya, maji na elimu vinaboreshwa huku akisisitiza kuboresha
elimu kutoka ngazi ya elimu ya msingi hadi sekondari kwa kuwataka pia wazazi
kupeleka watoto wao shule na kuwapatia mahitaji muhimu ili mtoto aweze kusoma
vizuri.
“Uwezo wa kuongoza na kushughulikia matatizo ya wananchi wa
kata hii ninao, kinachotakiwa hapa ni kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze
kujipatia maendeleo na kuweza kuondokana na umasikini”, alisema Nyandindi.
Vilevile alieleza kuwa ili kuweza kuleta mafanikio katika
hayo, atahitaji ushirikiano wa kutosha na usimamizi mzuri wa pamoja katika
kusimamia maendeleo ya wananchi, ili kuleta ufanisi wenye tija katika jamii.
Alifafanua kuwa kutokana na taaluma yake aliyonayo ya
uandishi wa habari, atawaunganisha akina mama, wazee na vijana kwa kuwapa mbinu
za kuunda vikundi vya ujasiriamali ili baadaye waweze kukopesheka na taasisi za
kifedha hatimaye waweze kusonga mbele, na kuepukana na tabia ya kuwa tegemezi.
“Katika safari hii ninaimani peke yangu siwezi kufika, lakini
wanaccm wenzangu ninawaomba waniunge mkono ili niweze kuingia madarakani na kuleta
mabadiliko ya kweli kwa kutekeleza mambo mbalimbali ya kimaendeleo, katika kata
yangu ya Mbinga mjini A”, alisema.
Nyandindi anaongeza kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kugombea
nafasi hiyo, ilitokana na kuchoshwa na viongozi waliokuwepo madarakani kwa muda
mrefu kutoa ahadi ambazo hawazitekelezi, na wananchi wakiendelea kuteseka.
No comments:
Post a Comment