Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
HALI ya kisiasa wilayani mbinga mkoa wa Ruvuma, si shwari au
kwa maneno mengine imechafuka ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo, kimeingia
katika hali tete kufuatia baadhi ya wanachama wa chama hicho wilayani humo,
kuvamia katika eneo la ofisi za chama hicho na kuutaka uongozi wa CCM wilaya
kutangaza matokeo ya uchaguzi kura za maoni kwa nafasi ya ubunge, kufuatia matokeo ya nafasi hiyo kukaa
muda mrefu kwa siku mbili, bila kutangazwa.
Aidha kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi wilayani humo
limeonekana askari wake wakidhibiti hali hiyo huku wengine wakionekana kubeba silaha
za moto, na mabomu ya machozi.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho wameendelea kuandamana maeneo
mbalimbali ya mji wa Mbinga, wakitishia kutoondoka katika maeneo ya ofisi za CCM
na kuonekana kuranda randa wakitamka maneno…………….“hapa mpaka kieleweke, tunachotaka
ni matokeo na sio vinginevyo”.
Hali hiyo imejitokeza leo kufuatia kutotangazwa kwa matokeo
ya kura za maoni ya chama hicho tawala kwa muda wa siku tatu sasa, ambao
umefanyika mapema Agosti Mosi mwaka huu, kwa jimbo la Mbinga mjini na Mbinga
vijijini.
Duru za siasa mjini hapa kutoka makao makuu ya Ofisi za CCM
wilayani humo, zinasema katika majimbo hayo Mbinga mjini mpaka sasa linadaiwa
kuongozwa kwa kura za maoni na Sixtus Mapunda, kati ya wagombea watatu
waliokuwa wakiwania nafasi hiyo na vijijini, Martin Msuha ambaye naye alikuwa
akishindana na wagombea wenzake nane.
Sinto fahamu inaendelea kutawala katika eneo la ofisi za CCM
wilaya ya Mbinga, na kutishia muendelezo wa amani katika eneo la ofisi hizo, ambapo
wanachama wa chama hicho wanaonekana kujawa jazba na kuutaka uongozi husika
utangaze matokeo ya nafasi hiyo ya ubunge, kutokana kucheleweshwa kutangazwa.
“Tunataka matokeo, tunataka matokeo, tunataka matokeo hapa
mkitaka amani tuleeteeni matokeo vinginevyo tunarudisha kadi za CCM hatukitaki chama
tunataka haki itendeke kwa mshindi aliyeshinda”, hayo ni maneno ambayo yalikuwa
yakitawala katika eneo la ofisi kuu za chama hicho wilayani humo.
Kadhalika licha ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa
Ruvuma, Verena Shumbusho kujitokeza mbele ya hadhira ambayo ilionekana kudai
matokeo hayo katika viwanja vya chama hicho, bado wanachama walionekana kujawa
jazba wakitamka maneno ya kutaka matokeo yatangazwe na wengine wakiendelea
kutamka maneno hawawezi kuondoka mpaka kieleweke.
“Ndugu zangu tulizeni jazba, lazima tufuate utaratibu wa
chama, hatuwezi kuendesha chama kwa mashinikizo”, alisikika akisema Shumbusho
mbele ya umati huo uliokuwa kwenye viwanja vya CCM mjini hapa.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho waliendelea wakisema,
wanamashaka na viongozi wa wilaya hiyo wakiwemo chama na serikali, huenda
wanapanga mpango wa kutaka kuyachakachua matokeo ili atangazwe mgombea ambaye
sio chaguo sahihi la wananchi.
Mpaka sasa habari hizi zinaingia katika mtandao huu, hali ni
tete katika eneo la ofisi za CCM wilayani Mbinga, kutokana na umati mkubwa wa
watu ukiendelea kutawala katika eneo hilo huku askari polisi wakiendelea
kuimarisha ulinzi na kutaka matokeo yatangazwe haraka, kutokana na
kucheleweshwa kutangazwa.
Waandishi wa habari ambao walikuwa wakishuhudia juu ya sakata
hilo na kumtaka Katibu wa wilaya hiyo, Zainabu Chinowa azungumzie juu ya hali
hiyo alisema kuwa mpaka sasa wanashindwa kutangaza matokeo kutokana na baadhi
ya vituo viwili vya jimbo la Mbinga mjini, kesho Agosti 4 mwaka huu wanachama
wa CCM wanalazimika kurudia kupiga kura kwa nafasi ya udiwani na jimbo la
vijijini katika kata ya Kihangimahuka, kuwepo kwa utata juu ya matokeo ya
nafasi ya ubunge.
No comments:
Post a Comment