Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete. |
Na Mwandishi
wetu,
Mbinga.
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kikundi cha zaidi ya watu
40 wanaodaiwa kupandikizwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Gaudence
Kayombo, katika kijiji cha Ruanda kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kimewashambulia na kuwarushia mawe waandishi wa habari waliokwenda kijijini
hapo, kutekeleza majukumu yao ya kikazi.
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela amezungumza na
vyombo mbalimbali vya habari na kueleza kuwa tukio hilo lilitokea Agopsti 17
mwaka huu majira ya saa 6:30 kijijini humo, ambapo waandishi hao walivamiwa na
kikundi hicho akiwemo na Mwenyekiti wa kijiji, Deograsias Haulle kwa kupigwa na
kurushiwa mawe.
Alisema Mwenyekiti Haulle ameumizwa mdomoni na puani ambako
alipigwa na jiwe na mtu asiyejulikana na kwamba amepatiwa matibabu, katika
hospitali ya wilaya hiyo na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Msikhela aliwataja waandishi wa habari mkoani Ruvuma, ambao
walikumbwa na mkasa huo kuwa ni; Kassian Nyandindi anayeandikia magazeti ya
kampuni ya Businesstimes, Aden Mbelle na Pastory Mfaume kutoka redio Jogoo FM iliyopo
mkoani hapa.
Alisema kuwa hali hiyo ilijitokeza wakati wanahabari hao
walipokwenda kutekeleza majukumu yao ya kikazi, kuandika habari za tukio la
kufungwa kufuli Ofisi za kata ya Ruanda na baadhi ya wananchi, ambao majina yao
bado hayajapatikana.
Wakati walipokuwa wamekamilisha kazi yao wakijiandaa kurudi,
ndipo kundi hilo ambalo lilijitokeza ghafla liliwashambulia waandishi hao na
kwamba mwandishi wa habari Mbele, alipigwa jiwe katika eneo la usoni upande wa
kulia.
Kamanda huyo wa Polisi aliongeza kuwa hivi sasa wamefanikiwa
kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye ni Daniel Komba maarufu kwa jina la Gadaffi,
ambaye ndiye rafiki wa karibu na Gaudence Kayombo.
Pia Komba alihusika kwa kiasi kikubwa kuongoza kikundi hicho kinachotafsiriwa
kuwa ni cha wahuni, na kuleta vurugu hizo na kwamba wenzake aliokuwa
akishirikiana nao kwenye sakata hilo wanaendelea kutafutwa, ili wachukuliwe
hatua za kisheria.
Kayombo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa (NEC) akiwakilisha wilaya ya Mbinga, alipopigiwa simu na waandishi wa habari ili aweze
kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo ya kupandikiza genge hilo la wahuni ambalo
liliwadhuru waandishi wa habari na Mwenyekiti wa kijiji hicho, hakuweza kupatikana na simu yake ilikuwa
ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Vilevile Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga naye amethibitisha
juu ya tukio hilo na kusema; “nimemwagiza
OCD wa Mbinga, ahakikishe uchunguzi wa kina unafanyika na watuhumiwa
waliohusika katika tukio wanakamatwa na taarifa zaidi tutaendelea kuzitoa
baadaye ni wangapi, waliohusika katika jambo hili”, alisema Ngaga.
Aidha alipohojiwa kwa
niaba ya wenzake, mwandishi wa habari Nyandindi alisema kuwa yeye alinusurika
kupigwa lakini aliokolewa na mtendaji wa kata hiyo ya Ruanda, Dominick Komba
kwa kumhifadhi ndani ya nyumba yake ambayo ipo kijijini humo.
“Wakati kundi hili linawasili katika eneo la ofisi za kata
ambako sisi waandishi wa habari tulikuwa tunafanya mahojiano na viongozi wa
kata hiyo, ghafla tulijikuta tumezingirwa na kikundi hicho huku wengine
wakipaza sauti wakisema sisi ni wafuasi wa Mbunge Kayombo hatuhitaji waandishi
wa habari hapa kijijini kwetu ondokeni haraka sana, huku wengine wakileta
fujo”, alisema Nyandindi.
Kwa upande wa waandishi wa habari wa redio Jogoo, katika
kunusuru uhai wao walikimbia na kwenda kujificha nyumba jirani, zilizopo katika
kijiji hicho.
Nyandindi aliongeza kuwa vurugu hizo zinatokana na mvutano wa
kisiasa uliotawala katika kata hiyo ambao umesababishwa na Mbunge Kayombo,
kutokana na kudondoka kwenye uchaguzi wa kura za maoni kupitia tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ambao umefanyika hivi karibuni, hivyo kikundi hicho
kimekuwa kikiendeleza vurugu kijijini hapo na kusababisha kufunga makufuli
katika ofisi za serikali za kata ya Ruanda.
“Baada ya kujinusuru na mkasa huu, tulikwenda kuripoti kituo
kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga, tumefungua jalada la kesi lenye namba MBI/IR/1370/2015
ambapo tunaviachia kazi vyombo vya dola viendelee kutekeleza majukumu yake ili
sheria iweze kuchukua mkondo wake, ikiwemo watuhumiwa waliohusika na tukio hili
wakamatwe na kufikishwa Mahakamani”, alisema.
No comments:
Post a Comment