Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Jakaya Mrisho Kikwete. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mbinga
vijijini mkoani Ruvuma, wameandamana kuelekea kwenye Ofisi za chama hicho
wakipinga kurudiwa uchaguzi kura za maoni katika kata ya Kihangimahuka na Ruanda
wilayani hapa, kwa madai kwamba kufanya hivyo kunalenga kumbeba mgombea mmojawapo ambaye
aliangukia pua katika uchaguzi huo uliofanyika hivi karibuni, Agosti Mosi mwaka
huu.
Tukio hilo la aina yake limetokea leo majira ya
asubuhi katika makao makuu ya Ofisi za CCM wilaya, ambapo wanachama hao
walionekana kujawa jazba huku wakidai maamuzi ya kurudiwa kwa uchaguzi huo sio
sahihi na kwamba huenda ukakigawa chama na kuzua migogoro miongoni mwa
wanachama.
Hali ya kata hizo ambako uchaguzi uliamriwa urudiwe na Kamati
kuu ya chama hicho Taifa, hivi sasa imeendelea kuwa tete ambapo wanachama waliopo katika maeneo
hayo nao wameandamana kupinga uchaguzi huku wengine wakitishia kukihama chama.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa kata ya
Ruanda John Ndimbo alisema kuwa wao wanachokifahamu viongozi wa Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga, ndio wamekuwa chanzo cha migogoro kutokana na kumbeba mgombea, Gaudence Kayombo ambaye alishindwa kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni.
“Baadhi ya watumishi wa Halmashauri jana Agosti 12 mwaka huu, wameonekana majira ya usiku wakipita
nyumba kwa nyumba kushawishi wanachama wampigie kura Kayombo huku wakidaiwa kugawa
fedha shilingi 5,000 na vifaa vya ujenzi kama vile bati, mifuko ya saruji na nondo jambo hili binafsi linanishangaza sana sisi tunachotambua
uchaguzi kura za maoni ulikwisha fanyika”, alisema Ndimbo.
Naye Hallad Ndimbo ambaye ni Katibu wa CCM kata ya
Kihangimahuka, alisema taarifa za kurudiwa kwa uchaguzi huo zinamshangaza na kwamba
yeye hatashiriki katika zoezi hilo ambalo kimsingi linaonekana kushinikizwa na
baadhi ya vigogo wachache, ngazi ya Halmashauri ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wilayani
humo, Christantus Mbunda alifafanua kuwa haki haijatendeka kuhusiana na kurudia
kwa uchaguzi huo, kutokana na wagombea wengine kutokuwepo huku akiongeza kwamba
ili haki itendeke ni lazima wote kwa pamoja wawepo, ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa
ya lazima.
Mbunda alieleza kuwa yeye binafsi anachofahamu uchaguzi
ulikwishafanyika kwa haki ambapo kwa kata hizo mbili za Kihangimahuka na
Ruanda, baadhi ya watu waliingilia akiwemo yeye mwenyewe mgombea Kayombo na
kuharibu mfumo wa matokeo ya kura za maoni, ambayo yalikwisha pigwa na wapiga
kura.
“Kama kurudia uchaguzi ni vyema ukarudiwa jimbo zima na sio
kwa kata mbili ambako anatokea mgombea, tunaiomba kamati kuu ya CCM Taifa kwa nia
njema kabisa na kwa manufaa ya chama chetu itende haki kwa wagombea wote”,
alisema Mbunda.
Aliongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni kizuri na watanzania
wengi wanakipenda, ila tu kuna watu wachache ambao wanamalengo ya kukiharibu
ikiwemo kung’anga’nia madarakani, hata kama wanachama na wananchi hawawataki.
Mbunda alisema wakati umefika kwa wale wote wenye tabia ya
kung’ang’ana na madaraka, waache tabia hiyo badala yake wakubali matokeo kwani
kufanya hivyo kutasaidia kujenga chama na kuondokana na kero mbalimbali, zinazosababisha migongano baina ya wanachama na viongozi.
No comments:
Post a Comment