Wananchi waliohudhuria mkutano wa CHADEMA Mbinga mjini eneo la soko kuu, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali. |
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Mbinga
mkoa wa Ruvuma, kimesema kitaendelea kujenga misingi ya kutetea na kupigania
haki na maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo, ili waweze kusonga mbele katika
nyanja mbalimbali za kimaendeleo na hatimaye waondokane na umasikini.
Aidha chama hicho kimeeleza kuwa, katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika
Oktoba 25 mwaka huu, watahakikisha wanashinda kwa kishindo kwa kuchukua viti
vingi vya udiwani na ubunge katika majimbo ya Mbinga vijijini na mjini, hivyo
wamewaomba wananchi waendelee kuwaunga mkono siku uchaguzi huo utakapofanyika
ili waweze kufikia malengo husika.
Kenan Mkuzo ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho wilayani
Mbinga, alisema hayo alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi waliokusanyika
kusikiliza mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya soko kuu,
mjini hapa.
“Ndugu zangu wanambinga naomba niwaeleze, wakati wa kuburuzwa
sasa umepita tunahitaji tupate viongozi bora watakaokaa madarakani na kuweza
kupigania maendeleo yetu kwa moyo wa dhati, hatuhitaji viongozi lege lege ambao
watalifikisha taifa hili mahali pabaya”, alisema Mkuzo.
Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na watu wengi na kufunika
viwanja hivyo, Mkuzo aliwaeleza wananchi kwamba kuna kila sababu kukichagua
CHADEMA kwa kukipigia kura nyingi kwa nafasi ya Udiwani, Ubunge na Rais ili kiweze kushika madaraka ya nchi hii na
kuweza kuleta maendeleo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
Pia katika mkutano huo, Wenyeviti wawili wa vitongoji kutoka tiketi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikihama chama hicho na kuhamia CHADEMA ambao
ni; Steven Mateso kutoka kitongoji cha Mbinga mjini A na John Kabuyuka wa
kitongoji cha Masumuni vyote vya mjini hapa.
Wenyeviti hao kwa nyakati tofauti mara baada ya kukabidhiwa
kadi za CHADEMA waliapa kwamba, watahakikisha wanashirikiana kwa pamoja kwenye uchaguzi
mkuu ujao chama hicho kinapata viti vingi vya uongozi.
Vilevile Katibu Mwenezi wa kata ya Lukarasi, Nestory Kapinga Mbinga
vijijini naye alirudisha kadi ya CCM na kuhamia Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo, huku akisema kuwa amechukua maamuzi hayo kutokana na kuchoshwa na
sera za Chama cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment