Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.
MWITO umetolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kuongeza juhudi katika masomo yao na
kujiepusha kushiriki vitendo viovu vinavyoweza kukatisha ndoto yao ya kujiendeleza
kimasomo kama vile kwa wanafunzi wa kike kupata mimba wakati wakiwa na umri
mdogo, au virusi vya Ukimwi.
Aidha wametakiwa kuwa na dhamira ya kweli juu ya kusukuma
maendeleo ndani ya wilaya yao, ili watakapohitimu masomo yao na kupata ajira
warudi kwenye maeneo yao kuwatumikia wananchi na sio kwenda kufanya kazi katika
mikoa au wilaya zingine ambako tayari wamepiga hatua kimaendeleo.
Imeelezwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kupunguza tatizo la
watumishi, hasa kwa idara ya afya, elimu na kilimo ambako mahitaji ya watumishi
wake ni makubwa.
Tekra Nyoni ambaye ni Afisa mipango wilaya ya Namtumbo,
alisema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akikagua ujenzi wa vyumba vya
maabara shule ya sekondari Chengena na Luchili wilayani humo, ikiwa ni
utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kutaka kila shule ya sekondari
hapa nchini kuwa na vyumba vitatu vya maabara, kwa lengo la kutoa fursa kwa
wanafunzi wa shule hizo kusoma masomo ya sayansi kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Nyoni, alisema kuwa wilaya hiyo inakabiliwa na
upungufu mkubwa wa vyumba vya maabara na watumishi katika sekta hiyo ya elimu.
Afisa mipango huyo amewataka wanafunzi wa kike kuwa na moyo
wa uvumilivu ikiwemo kukataa kurubuniwa na wanaume wenye tamaa ya ngono, ili
waweze kuepukana na kupata mimba zitakazosababisha kukatisha masomo yao na
badala yake muda mwingi wajikite katika masomo yao darasani.
No comments:
Post a Comment