Thursday, August 13, 2015

WATAKIWA KUJITOKEZA KUHAKIKI MAJINA YAO KATIKA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA

Mgombea ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini, Manjolo Kambili akionesha baadhi ya kadi za CCM ambao waliamua kuukana uanachama wao na kuamua kujiunga na Chama cha wananchi CUF.
Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenda katika vituo vyao walivyojiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ili wajiridhishe na kuhakiki kama majina yao, yameorodheshwa katika daftari hilo.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu wa Chama cha wananchi CUF wilayani humo, Abdalah Rajabu Abdalah wakati alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara wa kuwatambulisha wagombea udiwani na ubunge, uliofanyika viwanja vya baraza la Idd mjini hapa.

Alisema kuwa katika tukio hilo la uhakiki wa majina hayo, tume ya uchaguzi nchini imetoa muda wa siku tano tu, hivyo ni muhimu wakaenda mapema kufanya uhakiki wa majina yao ili wasikose haki yao ya kumchagua kiongozi wanayemtaka katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.


Alifafanua kuwa kwa mwananchi ambaye jina lake hataweza kuliona katika daftari hilo, atatakiwa kuwaona wahusika katika kituo na kuomba fomu ya kukata rufaa kwa Mratibu au msimamizi wa kata kwenye kituo husika, ambacho alijiandikisha.

Katibu huyo wa CUF alisema kuwa amelazimika kutoa tamko hilo, akiamini kwamba wapo watu ambao wamekatwa majina yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo baadhi yao kujiandikisha zaidi ya mara moja, au taarifa za muhusika hazikujitosheleza.


Hata hivyo alibainisha kuwa kutokana na tume kutambua uwepo wa matatizo mbalimbali, imeweka watu wa kuyatatua hayo ikiwemo pamoja na msimamizi wa kituo au kata husika ambao ndiyo wenye mamlaka ya kutolea ufafanuzi na maelezo ya vyanzo vilivyosababisha kuondolewa kwa majina, katika daftari hilo la kudumu la wapiga kura.

No comments: