Cresensia Kapinga. |
Na Muhidin
Amri,
Songea.
MWANDISHI wa habari mwandamizi, Cresensia Kapinga (40)
ameibuka kidedea baada ya Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya
Ndilimalitembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kumchagua kwa kura nyingi kupitia kura za
maoni zilizofanyika hivi karibuni, kuwa mgombea kwa nafasi ya udiwani kupitia
tiketi ya chama hicho Oktoba 25 mwaka huu.
Kapinga amefanikiwa kupata kura 527, dhidi ya wagombea
wenzake Hashimu Fungafunga aliyepata kura 127, Francis Lungu kura 111 na Issa
Kiwaneke aliyepata kura 27 ambapo huyu ni mwandishi wa pili mkoani hapa
kushinda kwenye mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Mbali na Kapinga mwandishi wa habari mwingine ni, Dustan
Ndunguru ambaye naye ameshinda kupitia mchakato huo wa kura za maoni kwa nafasi
ya udiwani katika kata ya Kihungu, wilayani Mbinga mkoani humo.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Kapinga
alieleza kuwa iwapo atachaguliwa kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba
mwaka huu, atahakikisha anapambana na watu wote hususani watumishi wa umma
ambao wanakwamisha kwa makusudi maendeleo ya wananchi wake, katika kata ya
Ndilimalitembo.
Kapinga alifafanua kuwa amelazimika kutoa kauli hiyo,
kufuatia baadhi ya wanachama wa chama hicho ambao walifurika katika ofisi za
CCM kata ya Ndilimalitembo, kumpongeza kwa ushindi alioupata huku wengine
wakisema sasa wanamatumaini mapya kwa mgombea huyo na kuanza kumpatia majukumu
ya kufuatilia mapato na matumizi ya miradi mbalimbali iliyotekelezwa ndani ya
kata hiyo, ambayo wananchi hawajasomewa na kupewa taarifa kamili juu ya
utekelezaji wake.
Alisema suala la kuwasomea wananchi mapato na matumizi ya
fedha za miradi yao ni jambo la lazima na sio vinginevyo, hivyo watendaji wa
mitaa na kata kwa ujumla atahakikisha wanatekeleza hilo kwa wakati, ili kuondoa
malalamiko yasiyokuwa na msingi.
Pia aliwaomba wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kujenga
ushirikiano wa pamoja na kuhakikisha wanamchagua Diwani, Mbunge na Rais wa CCM
kwenye uchaguzi mkuu ujao huku wakiacha ushabiki ambao unaweza kukiweka chama
pabaya.
No comments:
Post a Comment