Thursday, August 13, 2015

HATIMAYE KAMATI KUU YA CCM TAIFA YATENGUA MAAMUZI YA KURUDIA UCHAGUZI MBINGA VIJIJINI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jakaya Kikwete, akiwa pamoja na Katibu mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

HATIMAYE Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, leo imetengua maamuzi ya kurudia kufanya uchaguzi wa kura za maoni katika kata ya Kihangimahuka na Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kufuatia vurugu zilizoendelea kushika kasi Ofisi za CCM wilayani humo kwa masaa kadhaa, ikidaiwa kwamba kurudiwa kwa uchaguzi huo kunalenga kumbeba mgombea mmojawapo ambaye alishindwa katika uchaguzi wa kura hizo zilizofanyika, Agosti Mosi mwaka huu.

Aidha maamuzi hayo yalifikiwa leo jioni hii, baada ya Kamati ya siasa ya wilaya hiyo kuketi kwa muda wa masaa matano wakijadili suala hilo ikiongozwa na Katibu wa CCM mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho kufuatia wanachama wa chama hicho baada ya kuandamana kuelekea kwenye Ofisi za Chama wilaya, kupinga kurudiwa kwa uchaguzi huo kwenye kata hizo.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbinga, Christantus Mbunda alisema hayo mbele ya wanachama wa chama hicho ambao walikusanyika kwenye viwanja vya chama hicho, kusubiri hatma ya majibu hayo yaliyotolewa na Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi.

“Ndungu zangu wananchi wa Mbinga, kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa na kamati kuu ya chama baada ya kuketi na kujadili suala hili, wamekubaliana kwamba hakuna uchaguzi utakaoendelea kufanyika, hivyo endeleeni na shangwe na vifijo msilete fujo”, alisema Mbunda.


Mbunda mara baada ya kusema hayo, ndipo wanachama hao walipoanza kupiga vigelegele na wengine wakitamka maneno; “hatumtaki Kayombo tumechoka kuonewa, uchaguzi hapa haurudiwi tunataka maamuzi sahihi kama haya……………”

Wengine walikuwa wakisema kwamba wanahitaji busara ndani ya chama, hawataki kuburuzwa wanaheshimu msimamo wa matokeo yaliyotangazwa awali wakati uchaguzi huo wa kura za maoni, ulipofanyika hivi karibuni.

“Kayombo wamembeba, habebeki gari ya chama hapa haitoki kwenda Kihangimahuka na Ruanda kufanya kazi ya uchaguzi”, walisema.

Awali baada ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma, Verena Shumbusho kuwasili kwenye viwanja vya makao makuu ya Ofisi za CCM wilayani hapa, majira ya saa 7:27 na gari lenye namba za usajili DFP 7528 hali ilizidi kuwa tete katika eneo la ofisi hizo, waandamanaji waliokusanyika kwenye maeneo hayo kupinga kurudiwa kwa uchaguzi huo, walionekana kujawa jazba wakirudia kutamka maneno hatumtaki Kayombo, Msuha ni Jembe.


Jeshi la Polisi wilayani Mbinga, askari wake walionekana kuendelea kuimarisha ulinzi katika eneo hilo la ofisi za chama wilaya huku wengine, wakiwa wamebeba silaha za moto na mabomu ya machozi wakihakikisha amani na utulivu vinaendelea kutawala.


Hata hivyo CCM kwa upande wa Jimbo la Mbinga vijijini kulikuwa na wagombea ubunge nane ambao waliingia kwenye mchakato huo wa kura za maoni uliofanyika hivi karibuni ambao ni; Martin Msuha aliyeongoza kwa kupata kura (13,354), Gaudence Kayombo (12,068), Humprey Kisika (545), Dokta Silverius Komba (1,289), Edesius kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga (3,941) na Deodatus Ndunguru (7,060) matokeo hayo ambayo yalitangazwa Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku na katibu wa chama hicho wilaya ya Mbinga Zainabu Chinowa.  

No comments: