Abdulrahman Kinana. |
Na Muhidin Amri,
Nyasa.
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kukamilisha
mchakato wa kura za maoni hapa nchini, hali imekuwa si shwari kwa wilaya ya
Nyasa mkoani Ruvuma, ambapo baadhi ya wanachama wake wameonekana kukatishwa
tamaa kwa kile kinchodaiwa kuwa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Grayson Mwengu
amekuwa akitengeneza makundi ndani ya chama hicho wilayani humo, jambo ambalo
linahatarisha ustawi wake.
Kufuatia hali hiyo wanachama wa chama hicho walisema kuwa,
huenda CCM ndani ya wilaya hiyo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, kisifanye vizuri katika nafasi ya Diwani, Mbunge
na Rais kutokana na mambo yanayofanywa na katibu huyo ambayo yanaashiria
kukipeleka chama kubaya.
Walifafanua kuwa tayari baadhi ya wanachama wameanza
kujiondoa ndani ya chama na kujiunga na vyama vya upinzani, kwa kile
kinachoelezwa kuwa wamechoshwa na
vitendo vya dharau na kukosekana kwa umoja na mshikamano uliokuwepo kwa muda
mrefu na haya yote kukosekana huko, kumesababishwa na katibu huyo.
Kadhalika kwa nyakati tofauti Alex Shauri, Christopher Challe
na Steven Maluka walisema Mwengu, ni mtu mwenye kiburi na asiyependa
ushirikiano na wenzake ndani ya chama badala yake amekuwa na tabia ya
kuwakumbatia baadhi ya wagombea wenye fedha na kutotenda haki kwa wengine,
ambao wanaonekana hawana fedha jambo ambalo linalalamikiwa na wanachama wengi
wa chama hicho wilayani Nyasa.
Alex Shauri alieleza kuwa kutokana na hali hiyo kunauwezekano
mkubwa kwa CCM jimbo la Nyasa kutofanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, kwa kila alichoeleza kuwa baadhi ya
wanachama tayari wameonesha kukatishwa tamaa juu ya mwenendo na utendaji kazi
wa katibu huyo wilayani humo.
“Binafsi nasema kuna kila sababu kwa uongozi wa makao makuu
ya chama chetu kulifanyia kazi suala hili, hasa kuchukua hatua mapema kumuondoa
huyu mtu kabla hajakiharibu chama kwa kiasi kikubwa, wanachama tumekatishwa
tamaa na uongozi huu wa wilaya ndani ya CCM kila tunapofika ofisini kwake ni
mtu mwenye dharau, kiburi na amekuwa mtu ambaye hatoi ushirikiano wa kutosha”,
alisema Shauri.
Shauri ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu taifa (NEC) ya
Chama Cha Mapinduzi wilayani humo, ameendelea kuuomba uongozi husika ngazi ya
mkoa na taifa kwa ujumla kulifanyia kazi suala hilo, ili kuweza kukinusuru
chama ikiwemo kumuhamisha kituo hicho cha kazi katibu huyo ambaye muda mwingi
amekuwa akijigamba kwamba ameletwa Nyasa, kwa kazi maalumu na katibu mkuu wa
CCM Abdulrhaman Kinana.
“Yawezekana kweli ameletwa na bosi wetu Kinana, pamoja na
hilo sasa anachotakiwa ni lazima ajenge heshima na mahusiano mazuri na
wanachama wenzake, ukizingatia kwamba shughuli za chama zinahitaji mshikamano
wa pamoja”, alisema Shauri.
Naye Christopher Challe alisema kuwa tangu Mwengu alipoletwa
kufanya kazi wilayani Nyasa, amekuwa ni sehemu ya matatizo kwa kutengeneza
makundi na kuwagawa wanachama kitendo ambacho kinahatarisha ustawi wa chama na kukiweka
katika wakati mgumu.
Kwa upande wake waandishi wa habari walipomfuata Mwengu
ofisini kwake, ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo alikataa
kuzungumzia hilo, huku akiongeza kuwa yeye hana muda wa kuzungumza na vyombo
vya habari.
“Mimi kwa sasa sina muda wa kuzungumza na waandishi wa
habari, kwanza siwafahamu na mmetoka wapi au kawatuma nani”, alisema Katibu
huyo wa CCM wilaya ya Nyasa, akainuka katika kiti chake na kutoka nje ya ofisi yake
huku akiwaacha waandishi wa habari wakiwa wameshikwa na butwaa.
No comments:
Post a Comment