Na Steven Augustino,
Masasi.
UKOSEFU wa ushirikishwaji na utoaji wa elimu ya kutosha juu
ya uhifadhi shirikishi wa misitu ndiyo chanzo cha jamii, kuendelea kufanya
shughuli za uvunaji holela wa mazao ya misitu.
Kutokana na hali hiyo, wananchi wa kijiji cha Ulungu kata ya
Sindano wilayani Masasi mkoa wa Mtwara wameamua kufunga kwa muda usiofahamika
ufanyaji wa shughuli zote za uvunaji mazao ya misitu, hadi pale
watakapojiridhisha na maendeleo ya uoto wa asili katika msitu wa kijiji hicho.
Wananchi hao walibainisha hayo walipokuwa wakizungumza na
waandishi wa habari, ambao walitembelea kijijini hapo kutaka kujua mgawanyo wa
mamlaka na majukumu katika usimamizi wa misitu kati ya Meneja wa misitu wa
wilaya (TFS) na Afisa misitu wilaya (DFO) pamoja na kamati za maliasili za
vijiji.
Kwa nyakati tofauti wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa
kijiji hicho, Victor Athuman, Mathayo Patrick, Ahamad Machopa na mwakilishi wa
waganga wa tiba za asili kijijini hapo, Rukia Abdalah walisema pamoja na
kuundwa kwa kamati za maliasili lakini bado haijatolewa elimu ya kutosha kwa
wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji shirikishi wa misitu.
“Pamoja na kuwepo kwa kamati zinazosimamia utunzaji wa
misitu, lakini bado wananchi wa kijiji chetu hatuna elimu ya kutosha kuhusu
utunzaji wa misitu”, alisema Bi. Rukia.
Mwananchi mwingine aliyezungumzia matukio hayo, Victor
Athuman ambaye pamoja na mambo mengine alidai kuwa vitendo hivyo vimekuwa
vikichangiwa na umasikini mkubwa walionao wananchi wa kijiji cha Ulungu.
“Tatizo kubwa lililopo kwa wananchi wa kijiji hiki na hadi
tunafikia hatua ya kushambulia msitu tulionao, ni kutokana umaskini tulionao
tunakata miti ili tuweze kupata mbao tukaziuze tupate fedha, tunachoma mkaa na
matumizi mengine ili tuweze kuingiza kipato cha kuendeshea familia zetu”,
alisema Athuman.
Walisema bado elimu ya uhifadhi wa misitu ngazi ya vijiji
haijatolewa ipasavyo, jambo ambalo wananchi kwenye maeneo yao wamekuwa chanzo
kikubwa katika uharibifu wa rasilimali hiyo muhimu.
Ofisa maliasili wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi, Gabriel
Joshua licha ya kutolewa elimu kwa wananchi wa maeneo ya utunzaji na uhifadhi
shirikishi wa misitu, wananchi wamekuwa wagumu kupokea elimu husika.
“Tunajitahidi sana kutoa elimu kwa wananchi wetu pamoja na
kamati za maliasili za vijiji, lakini jamiibado haipokei elimuhiyo na badala yake wamekuwa
wakiendeleza vitendo vya uharibifu ikiwemo uvunaji holela wa misitu”, alisema
Joshua.
No comments:
Post a Comment