Na Steven Augustino,
Tunduru.
CHAMA cha wananchi (CUF)
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kimewataka wananchi wake kujipanga na kuweza
kufanya mageuzi ya viongozi katika uchaguzi mkuu ujao Oktoba 25 mwaka huu wa
kumchagua diwani, mbunge na Rais.
Katibu wa chama hicho
wilaya ya Tunduru, Abdalah Rajabu Abdalah alisema hayo alipokuwa
akiwatambulisha wagombea wa ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini, Manjolo Kambili
na kwa upande wa Tunduru Kusini, Sadick Songoni aliyeteuliwa na chama hicho
kupeperusha bendera kwenye jimbo hilo.
Huku akishangiliwa na
maelfu ya wananchi ambao walihudhuria kwenye mkutano huo, uliofanyika viwanja
vya baraza la Idd mjini hapa, Abdalah alisema kuwa chama hicho kimechukua
jukumu la kuwatambulisha wagombea hao ili wanachama waweze kuwafahamu, kabla ya
kuanza kwa mpambano wa kampeni Agosti 22 mwaka huu.
Akijitambulisha mbele ya
umati wa watu waliokusanyika kwenye mkutano huo, mgombea ubunge jimbo la
Tunduru Kaskazini, Manjolo Kambili aliwataka wananchi kujipanga kikamilifu na
kufanya mageuzi ya kweli katika uchaguzi huo.
“Ndugu zangu mwaka huu
hatuna pingamizi katika kufanya mabadiliko, tunachotakiwa hapa tufanye
mabadiliko ya kweli tuwang’oe hawa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi”, alisema
Kambili.
Naye Sadick Songoni
aliyeteuliwa kupeperusha bendera jimbo la Tunduru Kusini alipokuwa akiwasalimia
wananchi, mbali na kuwepo kwa ukweli kwamba anacho kibarua kigumu cha kumng’oa
Daimu Mpakate (CCM), akiwa anatumia sauti ya katibu mkuu wa CUF taifa, Maalim
Seif alitamba kuwa atamgaragaza mgombea huyo.
Wagombea hao walifafanua
kuwa katika mchakato wa kampeni hizo, wamejipanga kuwaeleza wananchi mambo
mengi ya ufisadi yaliyofanywa na viongozi wa chama tawala, katika nchi hii
tangu ipate uhuru miaka 54 iliyopita.
Akifunga mkutano huo
Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF wilaya ya Tunduru, Abdalah Mtalika alisema
endapo wananchi wa wilaya hiyo hawatabadilisha viongozi wa CCM katika majimbo
hayo, na kuweka viongozi kutoka vyama vya upinzania hawataweza kusonga mbele
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment