Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
DANIEL Komba (53) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ruanda kata
ya Ruanda mkoani Ruvuma, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya wilaya ya
Mbinga mkoani humo kwa kosa la kumshambulia Mwenyekiti wa kijiji hicho na
waandishi wa habari waliokwenda kijijini hapo, kutekeleza majukumu yao ya
kikazi.
Mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta, Seif Kilugwe alisema
hayo mbele ya Hakimu wa Mahakama ya wilaya hiyo, Issa Magori kuwa mshtakiwa
huyo alitenda kosa hilo Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 7 mchana.
Inspekta Seif alisema kwamba, Komba akiwa na wenzake
alimshambulia Mwenyekiti wa kijiji, Deograsias Haulle na kumjeruhi eneo la usoni
kitendo ambacho kilimsababishia maumivu makali mwilini mwake.
Alifafanua kuwa siku ya tukio kulikuwa na waandishi wa habari
wa mkoa wa Ruvuma, Kassian Nyandindi anayeandikia magazeti ya kampuni ya
Businesstimes, Aden Mbelle na Pastory Mfaume wa radio Jogoo FM nao walinusurika
kujeruhiwa katika vurugu ambazo zilizojitokeza kijijini hapo.
Mwendesha mashtaka huyo aliendelea kuieleza Mahakama kuwa,
hali hiyo ilijitokeza wakati wanahabari hao walipokwenda kutekeleza majukumu
yao ya kikazi, kuandika habari za tukio la kufungwa kufuli Ofisi za kata ya
Ruanda na baadhi ya wananchi, ambao majina yao bado hayajapatikana hivyo wakati
wakikamilisha kazi yao ya kuandika habari, ndipo walishambuliwa na kundi la
watu ambalo lilikuwa likiongozwa na mshtakiwa Komba.
Kadhalika aliongeza kuwa upelelezi shauri hilo bado haujakamilika
na kwamba watuhumiwa wengine ambao walihusika katika tukio hilo, bado
hawajapatikana wanaendelea kutafutwa na pale watakapopatikana watafikishwa
mahakamani ili waweze kujibu tuhuma inayowakabili mbele yao.
Hata hivyo mshtakiwa Komba alikana mashtaka, yupo nje kwa
dhamana ambapo shtaka hilo litatajwa tena mahakamani hapo Septemba 3 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment