Na Kassian
Nyandindi,
Ruvuma.
MGOMBEA urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dokta John Magufuli amesema kuwa, mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba 25
mwaka huu serikali itaanza mchakato wake wa kujenga barabara ya kutoka wilaya ya Mbinga kwenda Mbamba
bay wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kwa kiwango cha lami.
Sambamba na hilo alieleza pia serikali itaunganisha umeme wa
gridi ya Taifa kutoka Makambako mkoa wa Njombe hadi hapa Ruvuma.
Dokta Magufuli alisema hayo leo alipokuwa akihutubia mamia ya
wananchi wa wilaya hiyo, ambao walikusanyika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja
vya CCM mjini hapa.
“Ndugu zangu nataka niwahakikishie haya ninayosema nilazima
niyatekeleze, Tanzania ijayo ya Magufuli haitafanya mzaha juu ya kuleta
maendeleo ya wananchi, nchi hii najua ina fedha nyingi sana lazima zitumike
ipasavyo kwa manufaa ya jamii”, alisema Dokta Magufuli.
Alisema kuwa katika kufanikisha hilo, atahakikisha viongozi
ambao wanatabia ya kufuja fedha za wananchi anawachukulia hatua za kisheria
ikiwemo pia na kuziba mianya hiyo ya ufujaji, ili maendeleo yaweze kupatikana.
Kadhalika alifafanua kuwa endapo Watanzania watamchagua kwenda
Ikulu kuiongoza nchi hii, atawatumikia ipasavyo ili waweze kuwa na maisha bora
kwani waliowengi wamekuwa wakinyanyasika kutokana na kukosa haki zao za msingi.
“Nataka niwatumikie Watanzania waliowengi ambao
wananyanyasika, ndio maana leo hii nipo hapa nawaomba kura zenu kwa ajili ya
kuleta mabadiliko ya kweli, ninawaomba wanambinga tufanye mabadiliko yaliyobora
kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi ili Magufuli aweze kuwaletea maendeleo”,
alisema.
Pamoja na mambo mengine, mgombea huyo aliongeza kuwa anafahamu
wananchi wamekuwa na kero mbalimbali ambazo zinasababishwa na watumishi waliopo
madarakani katika Halmashauri za wilaya, mkoa hadi taifa hivyo atakapoingia
madarakani atawashughulikia ili kuweza kuondoa kero hizo.
No comments:
Post a Comment