Na Muhidin Amri,
Songea.
WAKAZI wa kijiji cha Namatuhi Halmashauri ya Songea vijijini
mkoani Ruvuma, watanufaika na kilimo cha umwagiliaji zao la mpunga baada ya
halmashauri ya wilaya hiyo, kukamilisha ujenzi wa skimu ya kilimo hicho.
Halmashauri ilichukua maamuzi ya kujenga miundombinu hiyo,
baada ya kuona wakazi hao wanashindwa kunufaika ipasavyo na shughuli za kilimo
cha zao hilo kutokana na kukosekana kwa miundombinu husika ya uzalishaji
mpunga, licha ya juhudi kubwa walizokuwa wakizifanya za uzalishaji wa zao hilo
kila mwaka.
Sixbert Kaijage, ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri
ya wilaya ya Songea vijijini alisema hayo wakati alipokuwa katika ziara yake ya
kikazi kijijini humo, akizungumza na wakulima wa zao hilo.
Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa, awali wananchi wa kijiji
cha Namatuhi walikuwa wakitumia njia za kizamani kuzalisha zao hilo kwa
kutegemea mvua za msimu, ambapo baada ya wananchi kuibua wazo la kutaka mradi
huo wajengewe miundombinu ya kisasa ya umwagiliaji, ndipo halmashauri hiyo
ikatekeleza hilo na sasa wanatumia njia bora za kilimo kuzalisha mapunga.
Kaijage alisema wilaya yake bado ina ardhi kubwa na yenye
rutuba inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali ya chakula na biashara, na
kwamba haitumiki vizuri kutokana na wakulima wengi kuendelea na kilimo cha
zamani cha kuhama hama huku akiwataka waanze kubadilika na kuachana na kilimo
cha mtindo huo ambacho hakina tija kwa karne hii ya sayansi na tekinolojia.
Aliongeza kuwa kuanzia msimu wa mwaka huu 2015 na 2016
atahakikisha wakulima wa wilaya ya Songea vijijini, wanatumia mbinu za kilimo
bora ili waweze kuzalisha kwa wingi mazao yao.
No comments:
Post a Comment