Katibu wa Halmashauri kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
GAUDENCE Kayombo ambaye ni mgombea nafasi ya ubunge kupitia tiketi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, amejikuta
akiendelea kuwa katika wakati mgumu kwa madai kwamba baadhi ya wananchi wa
kijiji cha Paradiso kata ya Ruanda kumfukuza kijijini hapo huku wakimwambia
kwamba, wananchi hawataki kusikia taarifa ya kurudia tena kufanya uchaguzi wa
kura za maoni katika kata hiyo.
Tukio hilo la aina yake limetokea usiku wa leo, Agosti 12
mwaka huu majira ya saa 2:20 wakati mgombea huyo akionekana katika maeneo ya
kijiji hicho akiwa na gari lake ikidaiwa anapita kwenye kata hiyo kuhamasisha
wapiga kura, wajitokeze kupiga kura ya maoni kwenye matawi yao kesho, Agosti 13
mwaka huu.
Hasira za wananchi hao zinafuatia baada ya CCM mkoani hapa,
kutoa taarifa kwamba kutafanyika marudio ya uchaguzi wa kura za maoni katika
kata ya Ruanda na Kihangimahuka kwenye jimbo hilo, baada ya matokeo ya awali kufutwa
kwa sababu mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni
kwenye jimbo hilo.
Marudio ya uchaguzi huo yanatokana pia na Kayombo kulalamikia
juu ya hali hiyo kutoridhishwa nayo, huku wagombea wenzake wakibaki kumshangaa
wengine wakisema amekosa kazi ya kufanya na huenda ni tamaa ya madaraka
aliyonayo au hajakomaa kisiasa.
Nimezungumza na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kata ya
Ruanda, John Ndimbo amethibitisha kutimuliwa kwa Kayombo katika kijiji hicho
usiku wa leo na kuongeza kuwa, yeye hana taarifa kamili juu ya marudio ya
uchaguzi huo.
“Hivi sasa ninavyokuambia dakika 20 zilizopita, Kayombo
amefukuzwa na wananchi wa kijiji cha Paradiso baada ya kukutwa akihamasisha kwa
mmoja wa katibu tawi, kwamba kesho kutafanyika marudio ya uchaguzi wa kura za
maoni katika kata hii,
“Wananchi walishikwa na hasira baada ya kumuona na kumwambia
hawataweza kupiga kura tena na hawamtaki, wengine walianza kushika mawe na
fimbo za miti wakitaka kupiga gari lake na hatimaye aliondoka na kutokomea
kusikojulikana’, alisema Ndimbo.
Ndimbo alisema wanamshangaa Kayombo akipita kuhamasisha watu
wapige kura wakati kazi hiyo ni ya viongozi wa chama na sio mgombea, hivyo
wanamashaka naye huenda anatamaa ya madaraka.
Kadhalika uchunguzi uliofanywa na mtandao huu, kwa upande wa
kata ya Kihangimahuka ambako uchaguzi unatarajiwa kurudiwa hali imekuwa tete
ambapo katibu kata wa CCM wa kata hiyo, Hallad Ndimbo amezungumza na mwandishi
wetu akisema kuwa wananchi hawapo tayari juu ya suala hilo.
“Binafsi sina taarifa kamili juu ya marudio ya uchaguzi huu
wa kura za maoni katika kata yangu, nasikia tu taarifa za mtaani ambazo sio
rasmi labda kama ningepewa hata barua na uongozi wa chama wilaya, ningeweza
kuzungumzia ukweli juu ya jambo hili”, alisema Ndimbo.
Kwa upande wake alipotafutwa mgombea, Kayombo ili aweze
kutolea ufafanuzi juu ya mkasa huo aliokumbana nao katika kijiji cha Paradiso
na viongozi hao wa CCM katika kata hizo, hakuweza kupatikana na simu yake
lilikuwa ikiita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
Pamoja na mambo mengine Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoani
Ruvuma, Verena Shumbusho alipoulizwa kwa njia ya simu na mwandishi wa habari
hizi juu ya kurudiwa kwa uchaguzi huo wa kura za maoni kwenye kata hizo kupitia
tiketi ya chama hicho, alithibitisha hilo akisema ni kweli kutafanyika marudio
ya uchaguzi huo kesho Agosti 13 mwaka huu.
Hata hivyo CCM kwa upande wa jimbo la Mbinga vijijini
kulikuwa na wagombea ubunge nane ambao waliingia kwenye mchakato huo wa kura za
maoni uliofanyika hivi karibuni ambao ni; Martin Msuha aliyeongoza kwa kupata kura
(13,354), Gaudence Kayombo (12,068), Humprey Kisika (545), Dokta Silverius
Komba (1,289), Edesius kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya
Kapinga (3,941) na Deodatus Ndunguru (7,060) matokeo hayo ambayo yalitangazwa
Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku na katibu wa chama hicho wilaya ya
Mbinga Zainabu Chinowa.
No comments:
Post a Comment