Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela. |
Na Steven
ASugustino,
Tunduru.
WATU watatu ambao ni wakazi wa mtaa wa machinjioni mjini
Tunduru mkoani hapa, wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha pikipiki
waliyokuwa wamepanda baada ya kugongana na lori.
Mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa ajali hiyo, ilitokea
kijiji cha Chingulungulu nje kidogo ya mji wa Tunduru.
Imeelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi aliokuwa
nao mwendesha pikipiki, ambaye alianguka ghafla mbele ya lori wakati akijaribu
kupita.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema
wanamshikilia dereva wa lori hilo anayefahamika kwa jina la Hassan Chimgege,
ambaye alijisalimisha polisi baada ya tukio hilo.
Msikhela aliwataja waliopoteza maisha kwamba ni wachimbaji wa
vito, ambao walitambulika kwa majina ya Peter Nyange na mwingine kwa jina la
Dotho Msukuma ambaye alikwenda mjini Tunduru, kwa lengo la kutafuta maisha
katika machimbo hayo.
Kadhalika mwingine aliyefariki katika ajali hiyo ni dereva wa
pikipiki hiyo, Yusuph Adam (30) na kwamba watu hao walikuwa wakitokea katika
machimbo yaliyopo mto Muhuwesi, wakielekea mjini humo kwa ajili ya kuuza madini
hayo ya vito.
Katika tukio hilo lori lenye namba za usajili T 669 ADV mali
ya Anton Onesmo mkazi wa mjini hapa, liliwagonga wapanda pikipiki hao ambao nao
walikuwa wakisafiria pikipiki yenye namba za usajili MC 703 ABV na kusababisha
vifo vyao papo hapo.
Mganga wa Hospitali wilaya ya Tunduru, Dokta Titus Tumbu
aliyeifanyia uchunguzi miili ya marehemu hao alibainisha kuwa chanzo cha vifo
vyao kilitokana na kutokwa na damu nyingi sehemu mbalimbali, baada ya kukumbwa
na mkasa huo.
Dokta Tumbu alifafanua kwamba marehemu Adam alipasuka fuvu la
kichwa na Peter alivurugika viungo vya ndani ya mwili wake, huku Dotho
akisagika mbavu zake zote kutokana kukanyagwa na magurumu ya gari hilo.
No comments:
Post a Comment