Na Muhidin Amri,
Ruvuma.
WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wamepewa changamoto ya
kutumia kalamu zao ipasavyo kwa ajili ya kuandika na kutangaza fursa mbalimbali
za maendeleo ndani ya mkoa huo, hatua ambayo itaweza kuwavutia wawekezaji wengi
wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza mkoani humo.
Mbali na hilo wametakiwa kutumia nafasi waliyonayo
kuhamasisha wananchi kupenda kushiriki katika shughuli za kimaendeleo, hususani
kwa zile za kujitolea ili kuweza kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla.
Chande Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani
Ruvuma, alitoa rai hiyo alipokuwa akikagua ujenzi wa chumba cha upasuaji akina
mama wajawazito kinachojengwa na serikali katika hospitali ya wilaya hiyo, huku
akiongeza kuwa ujenzi huo utatoa fursa kwa akina mama hao kuweza kupata huduma
za matibabu kwa ufanisi zaidi.
Nalicho alisema kuwa kazi ya kutangaza fursa zilizopo au
kuhamasisha wananchi kupenda kujiletea maendeleo siyo ya serikali pekee, bali
kila mmoja wakiwemo waandishi wa habari wanakila sababu ya kutumia kalamu zao
ipasavyo katika kuhamasisha jamii, ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kadhalika amewataka wanahabari mkoani humo kuandika habari za
uchunguzi kwani ndizo zinazoibua kero nyingi zinazoikabili jamii, badala ya
kutumia muda mwingi kuandika habari za wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo
wanaochangia kuleta umaskini na migogoro ya hapa na pale hususani kwa wananchi
waishio vijijini.
Hata hivyo amewasihi watumishi wa serikali na makundi mengine
katika jamii, kutobaki nyuma katika kupigania maendeleo bali kila mmoja
ahakikishe anakuwa chachu ya upatikanaji na mafanikio katika nyanja hiyo muhimu,
kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.
No comments:
Post a Comment