Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imepokea
kiasi cha shilingi milioni 345,213,000 kwa ajili ya kuwajengea uwezo watu
wanaoishi katika mazingira magumu na kuziwezesha kaya maskini kuongeza kipato,
ili waweze kuwa na uwezo wa kugharimia mahitaji yao muhimu katika maisha yao.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Nachoa Zakaria alisema hayo
alipokuwa akizindua zoezi la malipo kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya
maskini, kutoka mitaa mitatu ya kata ya Ruvuma wilaya ya Songea ambao
unatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu,
uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mapema mwaka huu.
Nachoa alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni
306,856,000 ni fedha za walengwa wenyewe, shilingi milioni 5,230,000 ambayo ni
sawa na asilimia 1.5 ni fedha zitakazokwenda ngazi ya mitaa kwa ajili ya
shughuli za usimamizi.
Kiasi cha shilingi milioni 3,477,000 zitatumika kwa ajili ya
usimamizi ngazi ya kata na shilingi milioni 29,639,500 zitatumika katika ngazi
ya halmashauri kwa ajili ya kazi kama hiyo ya ufuatiliaji na usimamizi, ambapo
tayari kaya 7,915 kutoka mitaa 53 zinaendelea kulipwa.
Awali mratibu wa TASAF katika Manispaa hiyo, Christopher
Ngonyani alisema kuwa ilikadiriwa kutambua kaya maskini 8,028 kutoka kwenye
mitaa hiyo baada ya kufanyika upembuzi wa kina, kaya zilizoibuliwa na kukidhi
vigezo zimefikia 7,915.
Ngonyani alisema fedha hizo zitatolewa kila baada ya miezi
miwili na mpango huo ni wa muda wa miaka mitatu, ambapo wanufaika amewataka
hasa akina mama kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa.
Mratibu huyo ameshauri pia kutumia fedha hizo wanazozipata,
kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) ili ziwasaidie kupunguza gharama kubwa ya matibabu, pale wanapougua.
No comments:
Post a Comment