Na Steven
Augustino,
Tunduru.
SEKRETARIETI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma,
imeridhia kumtoa katika mchakato wa kusimamia uchaguzi wa kura za maoni, katibu
wa chama hicho wilayani Tunduru mkoani humo, Mohamed Lawa ikiwa ni lengo la
kukiondoa chama katika mgogoro uliojitokeza kati ya katibu huyo na wagombea
ubunge jimbo la Tunduru Kaskazini.
Akitangaza maamuzi hayo hivi karibuni, Katibu wa Chama hicho
mkoani hapa, Verena Shumbusho alisema kuwa maamuzi hayo yamefikiwa baada ya
kujiridhisha uwepo wa hoja za msingi, zilizotolewa na wagombea hao.
Shumbusho alifafanua kuwa maamuzi hayo yametokana na sekretarieti
ya mkoa huo kuketi na kujadili hilo na kuchukua maamuzi ya kumteua Katibu wa
jumuiya ya wazazi mkoani Ruvuma, Haji Tajiri ambaye alikuwa miongoni mwao
kubakia Tunduru ili aweze kuendelea kusimamia mchakato huo hali ambayo iliweza
kuleta matumaini kwa wagombea na kukubali, kuendelea na mikutano ya kujinadi
katika jimbo hilo.
Akijibu maombi ya wagombea hao ya kukitaka chama kuchukua
hatua dhidi ya viongozi wote, watakaobainika kushiriki kugawa kadi za chama
pasipo kuwa na sifa pia waondolewe kwenye kinyang’anyiro cha kuwa mgombea kwa
nafasi ya udiwani au ubunge.
Zainabu Kalikalanje, Mussa Manjaule pamoja na makatibu wa
matawi wa CCM kutoka Nakapanya, Mchororo na Majengo wilayani Tunduru nao walitaka
wachukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kukiuka taratibu, sheria na miongozo
ya chama.
Shumbusho baada ya kupokea hilo, alisema atatuma kamati ya
maadili kwenda huko kwa ajili ya kulifanyia kazi.
Alisema kuwa katika mchakato huo, wagombea nane kati ya tisa
waligomea kuendelea na mchakato huo wakidai kubaini uwepo wa upendeleo wa
ugawaji kadi zisizokuwa halali kwa wanachama wa chama hicho wilayani humo,
ikiwa ni lengo la kutaka kumbeba mgombea waliyemtaja kwa jina la Injinia Ramo
Makani.
Katibu huyo alisema katika taarifa ya wagombea hao, ambayo
ilitumwa kwenda ofisi ya Chama Cha Mapinduzi mkoa na Taifa, ilibainisha kuwa
katika mgao wa kadi hizo kulikuwa na kata ambazo zilipewa kadi chini ya 200
huku matawi mengine yakipewa zaidi ya kadi 700 idadi ambayo ilikuwa hailingani
na uhalisia husika.
Alisema katika taarifa hiyo, makada hao walitolea mfano wa
mgao wa kadi 1000 ambazo inadaiwa kupelekwa kwenye tawi la Cheleweni, ambako
anatokea Injinia Ramo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, wagombea
hao Hassan Kungu, Issa Mtuwa, Omary Kalolo, Athuman Nkinde, Shaban Uronu, Moses
Kaluwayo, Michael Matomora na Rashid Mohamed walisema kuwa wapo tayari kumuunga
mkono mgombea yeyote miongoni mwao isipokuwa Injinia Ramo Makani.
No comments:
Post a Comment