Na Muhidin Amri,
Nyasa.
MAKADA tisa kati ya kumi kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, ambao waliangukia pua katika
mchakato wa kura za maoni kuomba ridhaa ya kugombea nafasi ya ubunge jimbo la
Nyasa, wamemnyoshea kidole katibu wa chama hicho wilayani humo Grayson Mwengu,
kuwa ndiye aliyechangia wao kushindwa vibaya katika mchakato huo.
Wanachama waliogombea nafasi hiyo na kushindwa kuwa ni
Christopher Challe, Ebehard Haule, Adolph Kumburu, Dokta Stephen Maluka, Frank
Mvunjapori, Alex Shauri, Gerome Mathayo, Cassian Njowoka na Oddo Mwisho walisema
katibu huyo wa chama alikuwa akimpendelea mgombea mwenzao Stella Manyanya
ambaye aliwashinda kwa idadi kubwa ya kura.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu; Alex
Shauri, Christopher Challe na Stephen Maluka walisema kuwa katibu huyo wa chama
wilaya hakuweza kutoa ushirikiano kwao, badala yake alikuwa akimkumbatia
mgombea mmoja na kuwasusa wengine.
Walisema kutokana na hali hiyo kuna uwezekano mkubwa kwa CCM
kutofanya vizuri katika uchaguzi mkuu ujao jimbo la Nyasa, kwa nafasi ya
udiwani na ubunge kwa madai kuwa baadhi ya wanachama tayari wameonesha kukata
tamaa juu ya mwenendo wa utendaji kazi, wa katibu huyo.
“Mimi nina imani kama hakutafanyika mabadiliko ya kumuondoa
katibu huyu wa chama wilaya, basi hatuwezi kupata ushindi katika jimbo hili la
Nyasa wanachama wamekatishwa tamaa na uongozi wa chama wilaya kwani kila
tunapofika ofisini kwake ni mtu mwenye dharau na kiburi, hataki kutupatia
ushirikiano”, alisema Shauri.
Shauri ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri kuu (NEC) ya Chama
Cha Mapinduzi wilaya ya Nyasa, ameuomba uongozi husika wa chama kuangalia
uwezekano wa kumwajibisha Mwengu kwani anaweza kusababisha chama kikashindwa
vibaya, katika uchaguzi mkuu ujao wilayani humo.
Naye Christopher Challe alisema tangu katibu huyo alipoletwa
na chama wilayani humo amekuwa ni mtu mwenye kujenga makundi, ambayo
yanahatarisha kukua kwa maendeleo ya chama.
Kwa upande wake Katibu wa CCM wilaya ya Nyasa, Mwengu
alipofuatwa ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo alikataa kuzungumza
huku akisema kwamba, hana muda wa kuweza kuzungumza na waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment