Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wametakiwa
kuwa na upendo, umoja na ushirikiano katika maisha yao ya kila siku jambo
ambalo litasaidia chama kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Aidha wamekumbushwa kuacha tabia ya kukatishana tamaa, kwani
hali hiyo inaweza kuwaamsha wapinzani wao kutoka kwenye vyama mbalimbali vya
kisiasa waweze kujipanga vizuri na kuleta ushindani mkubwa, kwa wagombea wa
Chama Cha Mapinduzi.
Rai hiyo ilitolewa na MKuu wa mkoa huo, Said Mwambungu
alipokuwa akizungumza na wanawake wa CCM kwenye mkutano mkuu wa uchaguzi wa
wabunge wa viti maalum, uliofanyika ukumbi wa Parokia ya Mtakatifu Theresia
Bombambili mjini Songea.
Mwambungu alisema chama hicho ni taasisi kubwa ambayo
haimtegemei mtu mmoja katika uendeshaji wa shughuli zake za kichama, hivyo si
jambo jema kuona mwanachama anajivua uanachama wake kwa sababu tu ya kushindwa
kwa mgombea ambaye alikuwa akimpigia kampeni, ili aweze kushinda katika nafasi
aliyoitaka.
Mkuu huyo wa mkoa amewahimiza wanaccm mkoani humo, kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo, ili kuwavutia watu wengine ambao
wanaweza kuhamasika na kujiunga na chama hicho.
“Ninyi mliopo hapa ni sehemu ya jamii huko muendako
mkashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya wananchi, kufanya hivi
mtaweza kukifanya chama kuwa na wanachama wapya wengi zaidi”, alisema
Mwambungu.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, alisema kuwa
upendo, umoja na mshikamano ndiyo silaha pekee itakayokiwezesha Chama Cha
Mapinduzi kupendwa, kuungwa mkono na watu wengine zaidi.
No comments:
Post a Comment