Na Kassian Nyandindi,
Songea.
ANDREW Kuchonjoma ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi
wa Habari mkoani Ruvuma (RPC) amewataka wanachama wake ndani ya klabu hiyo,
kujiendeleza kielimu katika tasnia ya habari ili waweze kufanya kazi zao kwa
urahisi, katika ulimwengu huu wa sayansi na tekinolojia.
Sambamba na hilo alieleza kuwa kuna kila sababu kwa mwandishi
wa habari kuzingatia maadili ya taaluma hiyo, wakati wa kutekeleza majukumu ya
kazi zake ya kila siku hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, ili kuweza
kuepukana na matatizo au migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.
“Ndugu zangu kusoma ni jambo muhimu sana ambalo tunapaswa
kulipatia kipaumbele, hapa Ruvuma kuna chuo cha habari ambacho nawashauri
wenzangu tujiunge na tuweze kupata fursa ya kujiendeleza kielimu tusiishie
kukaa tu bila kuwa na mawazo mapya ya kujiendeleza kielimu, katika taaluma hii
tuliyonayo”, alisema Kuchonjoma.
Kuchonjoma ambaye pia ni mwandishi wa habari mkongwe, alisema
hayo alipokuwa akizungumza na wanachama wa RPC mara baada ya kufanyika mkutano
mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho, uliofanyika hivi karibuni kwenye
ukumbi wa Ushirika uliopo mjini Songea.
Aidha kwa upande wake msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Mathew
Ngalimanayo ambaye ni Katibu mtendaji wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali
wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, aliwapongeza waandishi wa habari wa mkoa huo
kwa kujenga ushirikiano na kuendeleza mchakato wa kuanzisha redio ambayo
itamilikiwa na wanachama wa chama hicho mara itakapoanza kurusha mawimbi yake
hewani.
“Nimejifunza ninyi kweli mnao ushirikiano wa kutosha na
katiba yenu mnaisimamia ipasavyo katika shughuli za maendeleo ndani ya chama
chenu, nawaomba endeleeni kuwa wabunifu ninahakika mtafikia mahali pazuri kwani
kila jambo linamchakato wake, kinachotakiwa hapa ni kuendeleza mshikamano ili
mfikie malengo yenu mliyojiwekea”, alisema Ngalimanayo.
Pamoja na mambo mengine viongozi waliochaguliwa ambao
watakiongoza Chama cha waandishi wa habari mkoani humo, katika kipindi cha
miaka mitatu ambao ni; kwa nafasi ya Mwenyekiti ilichukuliwa na Andrew
Kuchonjoma, makamu Mwenyekiti, Marietha Msembele, Katibu mtendaji, Andrew
Chatwanga, Katibu mtendaji msaidizi Ngaiwona Nkondola, Mweka hazina Joyce
Joliga na msaidizi wake ni Alpius Mchucha.
Wajumbe wa kamati tendaji ni Kassian Nyandindi, Joseph
Mwambije, Mpenda Mvula na Geofrey Nillahi.
No comments:
Post a Comment