Cresensia Kapinga. |
Na Mwandishi wetu,
Songea.
CRESENSIA Kapinga ambaye ni mgombea udiwani kata ya
Ndilimalitembo, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) amesema atatumia nafasi hiyo ya uongozi mara baada ya kuingia
madarakani, kwa kuwatumikia wananchi ipasavyo wa kata hiyo hasa katika suala
zima la kusukuma mbele maendeleo yao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha Kapinga amewashukuru wanachama wa CCM ndani ya kata
hiyo, kwa maamuzi yao ya kumpatia heshima ya kugombea udiwani licha ya kukiri
kwamba mchakato wa kura za maoni kwa tiketi ya chama hicho ulikuwa mgumu, hivyo
atakapotimiza ndoto yake mara baada ya kuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi
mkuu Oktoba 25 mwaka huu, ataendeleza ushirikiano na wananchi wake katika
kutekeleza yale yaliyopo kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
“Endapo nitashinda kwenye kinyang’anyiro hiki cha uchaguzi
mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu, kubwa nitakalolifanya ni kutekeleza ilani ya
chama changu ili niweze kuwaletea wananchi wangu maendeleo kwa haraka zaidi”,
alisema Kapinga.
Alifafanua kuwa katika kutimiza majukumu husika na kuweza
kuleta ufanisi mzuri wa kimaendeleo, atahakikisha pia anatoa fursa sawa kwa
makundi yote ya kijamii ili kuweza kuleta mabadiliko ya kweli katika jamii.
Kapinga alisema hayo alipokuwa akihojiwa na vyombo mbalimbali
vya habari mjini Songea, huku akiongeza kuwa kwa mara ya kwanza aligombea
udiwani wa viti maalum mwaka 2010 kupitia CCM ambapo kura hazikutosha lakini
mwaka huu ameweza kujaribu tena na kufanikiwa kupitia chama hicho na kuwa
mgombea udiwani wa kata ya Ndilimalitembo, kwa kuwabwaga chini wagombea wenzake
watatu ambao waliingia kwenye kinyang’anyiro hicho kupitia kura za maoni.
No comments:
Post a Comment