Gaudence Kayombo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
MBUNGE wa Jimbo la Mbinga Gaudence Kayombo, ambaye aliingia
katika mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni jimbo la Mbinga vijijini mkoani
Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amewashangaza wanachama wa
chama hicho baada ya mbunge huyo kwenda ofisi za CCM wilayani humo kunyang’anya
vifaa vya matangazo, ambavyo ni vipaza sauti baada ya kushindwa kwenye kinyanga’nyiro
hicho cha kura za maoni uliofanyika Agosti Mosi mwaka huu.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti
mjini hapa, wanachama hao walisema kuwa Kayombo alifanya hivyo baada ya
kuwasili katika ofisi hizo za chama Agosti 14 mwaka huu majira ya asubuhi,
akionekana mtu mwenye hasira.
“Huyu Mbunge alipowasili pale ofisi za chama alitushangaza
sana, alikuwa mtu mwenye hasira huku akizungumza kwa ukali anataka vifaa vyake
vya matangazo ambavyo alikinunulia chama, huku akitamka maneno kwamba ameamua
kufanya hivyo kwa sababu viongozi wa chama wilaya hawamtaki”, walisema.
Aidha walifafanua kuwa kitendo alichofanya Kayombo ni cha
aibu, kwani yeye akiwa mwanachama wa CCM anapaswa kuendelea kukisaidia chama
kwa mambo mbalimbali na sio kufanya kitendo kama hicho, cha kunyang’anya vitu
ambavyo alikipatia chama.
Walibainisha kuwa Mbunge huyo baada ya kuona ameangukia pua
kwenye kinyang’anyiro cha kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni, muda
mwingi alikuwa akiwalaumu viongozi wa chama hicho wilaya ya Mbinga akisema kuwa
ndiyo waliochangia aweze kudondoka katika mchakato huo.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa
alithibitisha hilo na kueleza kuwa wao kama chama wamesikitishwa na kitendo
hicho ambacho hawakutegemea Kayombo kama angeweza kufanya hivyo.
“Huyu mtu ametushangaza sana, hili jambo alilofanya ni aibu
yake yeye mwenyewe tunajua kitendo hiki cha kutunyang’anya vipaza sauti ni
hasira zake alizonazo baada ya kushindwa, kwenye uchaguzi wa kura za maoni”,
alisema Chinowa.
Hata hivyo CCM kwa upande wa jimbo la Mbinga vijijini
kulikuwa na wagombea ubunge nane ambao waliingia kwenye mchakato huo wa kura za
maoni uliofanyika Agosti Mosi mwaka huu ambao ni; Martin Msuha aliyeongoza kwa
kupata kura (13,354), Gaudence Kayombo (12,068), Humprey Kisika (545), Dokta
Silverius Komba (3,941) na Deodatus Ndunguru (7,060) matokeo hayo yalitangazwa Agosti
3 mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku na Katibu wa Chama hicho wilaya ya Mbinga,
Zainabu Chinowa.
No comments:
Post a Comment