Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.
HATIMAYE mchakato wa kura za maoni kuwapata wagombea nafasi
ya ubunge katika majimbo mawili ya Tunduru kaskazini na Namtumbo hapa mkoani
Ruvuma, ambapo majimbo hayo yalichelewa kukamilisha mchakato huo kutokana na sababu
mbalimbali, hivyo ulifanyika tena mwishoni mwa wiki na wanachama wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kuwachagua Mhandisi Ramo Makani kuwa mgombea kwa jimbo la
Tunduru kaskazini na Edwin Ngonyani jimbo la Namtumbo.
Mchakato haukukamilika kwa muda uliopangwa kutokana na
kujitokeza kwa baadhi ya kasoro, ambazo zilisababisha wanachama walioshiriki
kugombea nafasi hiyo kugomea matokeo husika kwa madai kwamba walichezewa rafu
na wagombea wenzao.
Jimbo la Namtumbo uchaguzi kura za maoni ulilazimika kurudiwa
kutokana na kuwepo kwa madai ya idadi kubwa ya kura zilizopigwa, tofauti na wanachama
halisi waliostahili kupiga kura kitendo ambacho kililalamikiwa na wagombea
wengine waliokuwemo kwenye mchakato huo.
Wagombea hao waligomea matokeo yaliyomtangaza Vita Kawawa
kuwa ni mshindi, ambapo kwa mujibu wa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wilayani Namtumbo Aziz Fikiri alisema kutokana na kuwepo kwa malalamiko hayo
Katibu mkuu Taifa CCM, Abdulharman Kinana aliagiza kurudiwa kwa uchaguzi huo.
Agizo hilo lilionekana kuwa chungu kwa mshindi huyo wa
matokeo ya kwanza, ambaye naye alisusia kushiriki katika marudio ya uchaguzi
huo ambao ulifanyika kwenye baadhi ya maeneo, ambayo ni ngome kwa wagombea
wengine na maeneo ambayo Kawawa anakubalika, wapiga kura walikataa kurudia
kupiga kura.
Mbali na kususia kwa uchaguzi huo, Kawawa hakuweza hata
kuonekana ndani ya maeneo ya wilaya hiyo wakati uchaguzi ulipokuwa ukifanyika.
Pamoja na mambo mengine, jimbo la Tunduru Kaskazini uchaguzi
ulichelewa kufanyika kwa muda wa siku tatu kufuatia wagombea watano kati ya
sita ambao walishiriki katika kinyang’anyiro hicho cha kuomba ridhaa kwa tiketi
ya CCM kugombea nafasi ya ubunge katika jimbo hilo, walimkataa katibu wa chama
hicho wilaya ya Tunduru, Mohamed Lawa kwa madai kuwa alikuwa akimbeba mgombea
Ramo Makani ili aweze kurudi tena kwenye nafasi yake ya ubunge.
Hata hivyo katika uchaguzi huo wanachama wa chama hicho
kwenye jimbo hilo waliweza kumchagua tena Makani, kugombea ubunge jimbo la
Tunduru kaskazini baada ya kuwashinda wagombea wenzake.
No comments:
Post a Comment