Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
KUFUATIA vuguvugu la kisiasa ambalo limeendelea kushika kasi na
kutishia hali ya amani katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma, kutokana na wananchi kuutaka uongozi husika wa chama
hicho wilayani humo utangaze matokeo ya nafasi ya ubunge, hatimaye matokeo hayo
yalitangazwa kwa jimbo la Mbinga vijijini majira ya saa 5:45 usiku.
Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo kwa jimbo hilo, kulikuwa na
mvutano mkali ambao ulidumu kwa masaa 12, kutokana na kati ya wagombea nane
waliokuwa katika kinyang’anyiro hicho, mgombea Gaudence Kayombo kudaiwa kufanya
mchezo mchafu wa kutaka kuchakachua matokeo kwa kata ya Ruanda na
Kihangimahuka, ili yaweze kumpatia ushindi baada ya kuona hali ya upepo wa
ushindi kwa upande wake inamwendea vibaya.
Aidha kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi wilayani humo
lililazimika askari wake kuweka ulinzi mkali katika eneo la ofisi hizo za CCM,
kutokana na baadhi ya wanachama kuleta vurugu huku wengine wakirusha mawe.
Baadhi ya wanachama wa chama hicho waliendelea kuandamana maeneo
mbalimbali ya mji wa Mbinga, wakitishia kutoondoka katika maeneo ya ofisi za
CCM na kuonekana kuranda randa huku wakiimba nyimbo mbalimbali na kutamka
maneno…………….“hapa mpaka kieleweke, tunachotaka ni matokeo na sio vinginevyo”.
Sinto fahamu iliendelea kutawala katika eneo la ofisi za CCM
wilaya ya Mbinga ambapo wanachama wa chama hicho walionekana kuendelea kujawa
jazba na kuutaka uongozi husika utangaze matokeo ya nafasi hiyo ya ubunge,
kutokana kucheleweshwa kutangazwa.
“Tunataka matokeo, tunataka matokeo, tunataka matokeo hapa mkitaka
amani tuleeteeni matokeo vinginevyo tunarudisha kadi za CCM hatukitaki chama
tunataka haki itendeke kwa mshindi aliyeshinda”, hayo ni maneno ambayo yalikuwa
yakitawala katika eneo la ofisi kuu za chama hicho wilayani humo ambayo
yalikuwa yakitamkwa na wanachama wa chama hicho.
Kadhalika licha ya Katibu wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Ruvuma,
Verena Shumbusho kujitokeza mbele ya hadhira hiyo ambayo ilionekana kudai
matokeo hayo katika viwanja vya chama hicho, bado wanachama walionekana kujawa
jazba wakitamka maneno ya kutaka matokeo yatangazwe na wengine wakiendelea
kutamka hawawezi kuondoka mpaka kieleweke.
“Ndugu zangu tulizeni jazba, lazima tufuate utaratibu wa chama,
hatuwezi kuendesha chama kwa mashinikizo”, alisikika akisema Shumbusho mbele ya
umati huo uliokuwa kwenye viwanja vya CCM mjini hapa.
Baadhi ya wanachama waliendelea wakisema, wanamashaka na viongozi
wa wilaya hiyo wakiwemo chama na serikali, huenda wanapanga mpango wa kutaka kuyachakachua
matokeo ili atangazwe mgombea ambaye sio chaguo sahihi la wananchi.
Waandishi wa habari ambao walikuwa wakishuhudia juu ya sakata hilo
na kumtaka Katibu wa wilaya hiyo, Zainabu Chinowa azungumzie juu ya hali hiyo
alisema kuwa mpaka sasa wanashindwa kutangaza matokeo kutokana na jimbo hilo la
Mbinga vijijini katika kata ya Ruanda na Kihangimahuka, kuwepo kwa utata juu ya
matokeo ya nafasi ya ubunge.
“Ndugu zangu waandishi wa habari chama kimetuma magari huko
Kihangimahuka na Ruanda kufuatilia juu ya suala hili, kwa sababu matokeo
yanaleta utata kidogo, hivyo yakiletwa na chama kujiridhisha juu ya jambo hili
tutayatangaza muda wowote hata kama itakuwa ni usiku nawaomba wananchi waache
jazba wakati tunaendelea na mchakato huu”, alisema Chinowa.
Kadhalika baada ya kukamilika kwa taratibu husika za chama ndipo
matokeo kwa nafasi ya ubunge wa jimbo la Mbinga vijijini yalitangazwa Agosti 3
mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku ambapo, Martin Msuha aliweza kuchukua nafasi
ya ushindi katika jimbo hilo kwa kupata kura 13,354 na kuwagaragaza chini
wagombea wenzake saba, waliokuwepo kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wagombea wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo na kura
walizopata katika mabano kuwa ni; Humprey Kisika (545), Dokta Silverius Komba
(1,289), Edesius Kinunda (2,355), Deodatus Mapunda (2,532), Benaya Kapinga
(3,941), Deodatus Ndunguru (7,060) na Gaudence Kayombo aliyepata kura 12,068.
Pamoja na mambo mengine, wilaya ya Mbinga ambayo ina majimbo mawili ya
uchaguzi Mbinga mjini na vijijini ambapo kwa upande wa jimbo hilo la mjini
matokeo yake kwa nafasi ya ubunge yanatarajiwa kutangazwa leo majira ya jioni,
baada ya kumalizika kwa uchaguzi mdogo ambao unaendelea katika kata ya Kikolo
na Uzena zilizopo wilayani humo.
No comments:
Post a Comment