Na Mwandishi
wetu,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imewaasa
washiriki wa mafunzo ya uibuaji miradi kwa jamii kuwa wasikivu ili waweze kwenda
kutoa ushirikiano katika hatua zote zitakazotakiwa kutekelezwa wakati wa
utambuzi wa matatizo ya wananchi vijijini, hususani kwa yale yatakayolenga
kuinua kipato katika jamii.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tina
Sekambo alisema hayo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku saba kwa wataalamu 26
kutoka ngazi ya kata wilayani humo wanaojengewa uwezo, kuhusu utaratibu wa
kutekeleza miradi ya kutoa ajira kwa muda ambayo inatekelezwa chini ya mpango
wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na TASAF awamu ya tatu.
Sekambo alifafanua kuwa baada ya wataalamu hao kukamilisha
mafunzo hayo, watakwenda kuungana na wenzao 46 vijijini kwa ajili ya kubaini
fursa na kuibua miradi itakayotoa ajira za muda, hasa kwa uboreshaji wa
mindombinu kwenye maeneo yao huku walengwa hao wakinufaika kwa kuongeza kipato
chao.
Sambamba na maelekezo hayo Mkurugenzi huyo aliwataka
wataalamu hao kuzingatia, kuuliza, kusoma na kuwa wazi kwa mambo ambayo
hawatakuwa wanayaelewa ili kuwawezesha kujengewa uelewa, utakaowafanya waende
kutekeleza kazi hizo kwa weledi mkubwa.
Awali akisoma hotuba ya Mkurugenzi wa TASAF nchini, Ladslaus
Mwamanga Meneja miradi ya kutoa ajira ya muda kwa walengwa, Barnabas Jachi
alisema dhima kubwa ya uibuaji wa miradi hiyo inalenga kuimarisha miundombinu
ya uhifadhi wa udongo, uvunaji maji, kudhibiti makorongo na kuotesha vitalu vya
miti.
Jachi alifafanua kuwa mpango huo unafuatia uzinduzi wa mradi
uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, Agosti 15 mwaka 2012 na kuanza kutekelezwa
Februari mwaka 2013 ukiwa unalenga kunusuru kaya masikini.
Alisema kuwa baada ya mafunzo hayo washiriki hao watatakiwa
kuja na mikakati ya pamoja ambayo watakwenda kuelimisha jamii, ambapo malengo
na manufaa ya mpango huo ni kupunguza umasikini kwa wananchi waishio vijijini.
Pamoja na mambo mengine akizungumza kwa niaba ya washiriki
wenzake Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Omary Makina aliwatoa mashaka viongozi hao
kwamba huko waendako watatekeleza wajibu wao kwa moyo na kujituma kwa nguvu
zote, ili kuwawezesha wananchi waweze kufikia malengo yaliyowekwa na serikali
kupitia mpango huo.
No comments:
Post a Comment