Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Nyasa mkoa
wa Ruvuma, wametakiwa kuwa makini kwa kutokubali kutumiwa na wagombea
wanaowania nafasi ya ubunge wilayani humo hasa kwa wale ambao wamekuwa na tamaa
ya madaraka, badala yake jukumu lao kubwa ni kuwachuja ili kuona kama kweli
watakuwa na uwezo na moyo wa kuwasaidia wananchi, pale watakapokuwa wamepewa nafasi ya
kuwaongoza.
Aidha wametakiwa kuhakikisha kwamba, CCM kinapata ushindi wa
kishindo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu,
ambapo hilo litatokana na kujenga mshikamano wa dhati ikiwemo kutangaza kwa
wananchi yale yote yaliyotekelezwa kwa vitendo na chama hicho, kama
ilivyoainishwa ndani ya ilani yake ya uchaguzi.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa NEC wa wilaya ya Nyasa, Alex
Shauri alipokuwa akiwashukuru wajumbe wenzake wa Chama Cha Mapinduzi wilayani
humo, mara baada ya kumchagua kupeperusha bendera ya nafasi hiyo katika wilaya
hiyo.
“Ndugu zangu mwaka huu tuwe waangalifu sana, tuchague
viongozi bora kwenye kura za maoni katika chama chetu zinazotarajiwa kufanyika
hivi karibuni, tuwe waaminifu tusichague kiongozi ambaye baadaye tutashindwa
kumuuza kwa wananchi wakati uchaguzi mkuu utakapofanyika”, alisema Shauri.
Uchaguzi wa kumpata mjumbe wa nafasi hiyo ulifanyika Julai 6
mwaka huu kwenye ukumbi wa Bay Live uliopo mjini hapa, ambapo kinyang’anyiro
hicho kilikuwa na wagombea watatu ambao ni Ludwick Kumburu, Adam Mhaiki na Alex
Shauri.
Shauri aliweza kushinda kwa kishindo kwa kuwagaragaza wenzake
huku akiwaacha mbali kwa kupata kura 105, Kumburu alipata kura 16 na Mhaiki
kura 6.
Awali akizungumza na wajumbe waliohudhuria katika uchaguzi
huo mara baada ya kutangaza matokeo hayo msimamizi mkuu wa uchaguzi, Zainabu
Chinoa ambaye pia ni Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga mkoani hapa alisema vyama
vya upinzani, siku zote vimekuwa na kawaida ya kuwarubuni wanachama wa chama
hicho tawala kwa kuwadanganya wakiuke sheria za nchi, ikiwemo kuandamana bila
kibali halali huku wao wenyewe wakirudi nyuma jambo ambalo mwisho wake
husababisha kukumbana na matatizo makubwa, ikiwemo hata kupelekwa mahakamani.
Chinoa aliongeza kuwa wakati umefika sasa kwa wanachama wa
chama hicho kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, lakini
pia wahamasishe wale ambao sio wanachama wa CCM wajiunge ili kuongeza idadi ya
wanachama.
No comments:
Post a Comment