Wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wakiwa wamekusanyika pamoja kumsikiliza Kamanda wao wa Umoja huo, Cassian Njowoka. |
Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
ZIARA ya Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi
(UVCCM) wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, imeendelea kung’ara na kushika kasi
katika maeneo mbalimbali wilayani humo, kufuatia wanachama wa umoja huo
kujitokeza kwa wingi katika kila eneo la mapokezi yanapofanyika.
Njowoka ambaye anaendelea na ziara yake ya kikazi wilayani
humo, ikilenga kutembelea timu za mpira wa miguu na ambazo zinashiriki ligi kuu
ya UVCCM wilayani humo, maarufu kwa jina la Njowoka Cup pamoja na kuongea na
wanachama wa umoja huo.
Washiriki wa ligi hiyo amekuwa akiwapatia zawadi ya vifaa vya
michezo kama vile kikombe kimoja cha ushindi, jezi seti tatu na mpira mmoja kwa
mshindi wa kwanza, jezi seti mbili na mpira mmoja kwa mshindi wa pili na seti
moja ya jezi kwa mshindi wa tatu.
Haya yote yanajiri kufuatia ahadi yake aliyoitoa hivi
karibuni katika zoezi lake la kuwasimika makamanda wa UVCCM kwa kila kata za
wilaya hiyo.
Aidha licha ya kufanya hivyo, pia amekuwa akichangia vifaa
katika vituo vya afya na zahanati zilizopo wilayani humo ambapo vitanda,
mashuka ya kulalia, vyandarua kwa pamoja vimekuwa vikitolewa kwenye maeneo hayo
ili viweze kusaidia wananchi.
Wilaya ya Nyasa ambayo hivi sasa inakabiliwa na changamoto
kubwa katika huduma ya afya, Kamanda huyo wa UVCCM ameapa kuendelea kusaidia
katika sekta hiyo muhimu ili jamii iweze kuondokana na kero hiyo kwa kuchangia
shughuli za ujenzi na vifaa muhimu vya matibabu.
"Nitaendelea kusaidia ndugu zangu wa huku Nyasa, sisi sote tunapaswa kuungana ili tuweze kufikia malengo, wilaya yetu inachangamoto nyingi ambazo zinahitaji kuungana pamoja ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea", alisema Njowoka.
Hata hivyo ziara hiyo ambayo ilianza mapema Juni 25 mwaka huu
katika kijiji cha Ngindo kata ya Lipingo, anatarajia kuhitimisha mzunguko wake
kwa wilaya yote ya Nyasa ifikapo Julai 14 mwaka huu katika kijiji cha Ndondo
kata ya Liparamba wilayani humo.
No comments:
Post a Comment