Na Muhidin
Amri,
Songea.
WAZIRI wa maliasili na utalii, Lazaro Nyalandu ambaye pia ni
mmoja kati ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapa nchini ambao wanawania
kuteuliwa na chama hicho kugombea nafasi ya urais, amewatahadharisha viongozi
na wanachama wa CCM kuwa makini katika uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali
za uongozi, ili kuepuka kuteua watu wasiokuwa na sifa ambao watakuwa mzigo kwa
chama wakati utakapofika wa kuwanadi kwa wananchi.
Nyalandu alisema kuwa CCM imara itajengwa na viongozi imara
waliopo madarakani, kwa kuzingatia hekima na kusimamia vizuri misingi ya haki
na ukweli na kwamba pasipo kufanya hivyo wanaweza kukipeleka chama kubaya na
kusababisha baadhi ya wanachama, kushindwa kukiamini tena.
Waziri huyo aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na
baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Ruvuma, mara baada ya
kukamilisha zoezi la kuwapata wadhamini kwa nafasi hiyo anayogombea.
“Ninawatahadharisha wanaccm wenzangu, muda utakapofika msifanye
mchezo kwa kumchagua mtu ambaye atakuwa mzigo kwenu chagueni mtu ambaye licha
ya kuwa na uwezo wake wa kiutendaji ndani na nje ya chama, lakini awe muadilifu
na anayefahamu vizuri misingi na taratibu za nchi yetu”, alisema.
Alisema kwamba wakati wa kupokezana kijiti cha uongozi katika
nchi hii umefika, hivyo ni zamu ya watu wengine kuingia Ikulu kuendeleza yale
yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete, ambapo katika muda wa utawala wake kipindi
cha miaka kumi Rais huyo amefanya mambo mazuri ambayo leo hii Watanzania
wanajivunia.
Alifafanua kuwa ni jambo la kusikitisha kuona kuna baadhi ya
Watanzania ambao hawana shukrani, wamekuwa wakibeza mafanikio yalipatikana
katika uongozi huu wa awamu ya nne badala yake aliwataka waache kufanya hivyo,
kwani hukatisha tamaa.
Endapo atapata nafasi ya kupeperusha bendera kwa nafasi ya
urais katika nchi alisema, mambo ya msingi atakayoyaendeleza ni umoja, amani na
mshikamano kwa watu wote.
Kwa mujibu wa Nyalandu aliongeza kuwa yeye amekuwa ndani ya
CCM tangu akiwa na umri mdogo, ambapo hivi sasa licha ya kuwa waziri lakini ni
kati ya wagombea wachache waliozaliwa, kukua ndani ya chama na sio kama
ilivyokuwa kwa wagombea wengine ambao wamekikuta chama njiani.
No comments:
Post a Comment