Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
WANAHABARI mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia maadili ya
taaluma yao, kwa kujenga ukweli katika kazi zao za kila siku ambazo huripoti
katika vyombo vya habari, ikiwemo kufichua watu wanaojihusisha na vitendo vya
kuomba, kupokea na kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 25 mwaka huu.
Licha ya kufanya hivyo, wamehimizwa kujiendeleza kielimu
jambo ambalo litawafanya waweze kuwa na uwezo mkubwa wa kuandika habari hasa zile
za uchunguzi, ambazo husaidia jamii kuleta chachu ya kimaendeleo.
Pendo Ndumbaro ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake
(UWT) wilayani Mbinga, alisema hayo alipokuwa akifungua semina ya siku mbili
kwa akina mama wa umoja huo waliotoka katika kata zote za wilaya hiyo, yenye
kulenga kuwahamasisha na kuwajengea uwezo wanawake hao kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi.
Ndumbaro alisema ni jambo la kushangaza kumuona mwandishi wa
habari, anaacha majukumu yake ya kazi na kugeuka kuwa mpiga debe wa mgombea
fulani, huku akitambua fika kufanya hivyo ni kuvunja maadili ya kazi.
Aidha Mwenyekiti huyo alitumia nafasi hiyo, kuwakumbusha
waandishi wa habari kutangaza fursa zilizopo ndani ya mkoa wa Ruvuma, ambazo
kwa kiasi kikubwa zitasaidia kuvutia watalii wa ndani na nje.
“Mbali na hili vita dhidi ya vitendo vya rushwa ni lazima
muelimisha jamii kila kukicha katika vyombo vyenu vya habari, kwani kalamu zenu
zina nguvu kubwa kuliko upanga na huwafikia idadi kubwa ya watu kwa haraka
zaidi”, alisema.
No comments:
Post a Comment