Na Steven
Augustino,
Songea.
ROBERT Mkika (26) ambaye ni askari wa kikosi cha Jeshi la
Kujenga Taifa (JKT) Mlale mkoani Ruvuma, anatafutwa na Jeshi la Polisi mkoani humo
ili aweze kujibu tuhuma ya kumtesa mtoto wa ndugu yake, ambaye alikuwa akiishi
naye.
Mtoto huyo ambaye anafahamika kwa jina la Frank Kiria (9) anasoma
darasa la tatu katika shule ya msingi mkombozi, Manispaa ya Songea mkoani hapa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
amethibitisha juu ya tukio hilo na kueleza kuwa katika kuhakikisha mtoto huyo
anapata uangalizi salama hivi sasa wapo katika mchakato wa kufanya mawasiliano
na vituo vya kulea watoto yatima, ili waweze kumkabidhi huko hadi taratibu za kumrejesha
kwao Bukoba kwa wazazi wake zitakapokamilika.
Msikhela alifafanua kuwa Frank alikimbia nyumbani kwa askari
huyo wa JKT Mei 27 mwaka huu, na kwenda kwa rafiki yake Jackson Malekela
kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata.
Alisema rafiki yake huyo wote wanasoma darasa la tatu katika
shule hiyo, na kwamba Mama mzazi wa Jackson, Bi Bupe Mlawa baada ya kumpikia
chakula na kumaliza kula alipomtaka mtoto huyo arudi kwao, alikataa na kudai
kuwa hatarajii kurudi tena kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata.
Mama huyo alipofanya mahojiano naye, Frank alisema kwamba amekuwa
akinyanyaswa kwa kunyimwa chakula, mavazi na kulazwa chini mambo ambayo askari
polisi baada ya kupewa taarifa na mama Mlawa walijionea kipindi walipokwenda
kufanya uchunguzi, nyumbani alikokuwa akiishi mtoto huyo.
Taarifa za awali zinaonesha kuwa askari huyo wa Jeshi la
kujenga taifa, alikwenda kumchukua mtoto huyo huko Bukoba mwaka 2014, kwa madai
kuwa anakwenda kumlea.
No comments:
Post a Comment