Waziri Bernad Membe akipokelewa jana na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma, wakati alipowasili katika Ofisi za makao makuu ya CCM mkoani humo zilizopo katika Manispaa ya Songea. |
Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa,
Bernad Membe amesema iwapo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitampa ridhaa ya kugombea
nafasi ya Urais na kushinda katika uchaguzi mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba
mwaka huu jambo la kwanza atakalolifanya kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma, ni
kujenga viwanda vingi vitakavyosaidia kusindika vyakula kwa ajili ya kuongeza
thamani ya mazao yanayolimwa mkoani humo, ili wakulima wake waweze kukua
kiuchumi.
Hayo yalisemwa jana na Waziri Membe alipokuwa akizungumza na baadhi
ya wanachama wa CCM, alipokuwa katika harakati zake za kutafuta wadhamini ndani
ya chama hicho mkoani hapa, ambapo zaidi ya wanachama 5600 walijitokeza
kumdhamini mgombea huyo wa Urais.
“Namuomba sana Mungu endapo chama changu kitanipa ridhaa ya
kupeperusha bendera na hatimaye kushinda nafasi hii mwezi Oktoba, basi jambo la
kwanza nitakalowafanyia ndugu zangu wanaruvuma ni kujenga viwanda ili vyakula
vinavyolimwa hapa kwetu, viweze kusindikwa katika ubora unaokubalika”, alisema Waziri
Membe.
Aidha amewataka wanachama wa chama hicho kutowaogopa wagombea
wengine, ambao wameonesha dhamira ya kugombea urais kupitia tiketi ya CCM.
Waziri Membe alisema wanachopaswa ni kuwauliza maswali juu ya
uadilifu na uwajibikaji wao, kwa wananchi hatua itakayowawezesha kutambua nani
anafaa kusimamishwa na kugombea katika kinyang’anyiro hicho.
Kwa mujibu wa kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi, alisema
nafasi hiyo ya urais ni kubwa kuliko nafasi nyingine za uongozi hivyo sio ya
kuifanyia majaribio hasa pale linapokuja suala la mahusiano ya kimataifa,
ambapo wagombea wote wanaotaka kuchaguliwa na chama hicho na hata wale
watakaochaguliwa na vyama vya upinzani ni yeye tu ndiye mwenye sifa hiyo,
ikilinganishwa na wenzake waliotangaza nia ya kugombea nafasi hiyo.
Alisema baadhi ya wagombea wamekuwa mabingwa wa kuzungumza na
kutoa kauli zenye maneno matamu, yenye kuwavutia wanachama na wananchi kwa
ujumla ili wa wachague huku akisema wananchi wanapaswa kuwapuuza kwani hawana
jipya kutokana na utendaji wao mbovu walipokuwa watendaji wa umma, huku
akiongeza kuwa itakuwa sio vyema kuwapa ridhaa ya kuongoza nchi hii inayobeba
maisha ya Watanzania karibu milioni 48.
Akizungumza na umati wa wananchi nje ya ukumbi wa makao makuu
ya CCM mkoani Ruvuma uliopo mjini Songea, ambao walikusanyika kumpokea mara
baada ya kumaliza zoezi la kutafuta wadhamini katika mkoa huo, Waziri Membe alisema
endapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha pia nchi inaendelea kuwa na amani na
utulivu wakati wote wa utawala wake, ili kutoa nafasi kwa wananchi waweze
kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo bila usumbufu wa aina yoyote ile
katika maeneo yao wanayoishi.
Waziri huyo ameahidi kupunguza matumizi mabaya ya fedha za
walipa kodi, badala yake atazielekeza katika kujenga uchumi imara, huku
wananchi wake wakipewa kipaumbele katika kumiliki fursa za kiuchumi.
Mbali na hilo amewatahadharisha Watanzania kuwa makini na
kutokubali kuvurugwa na baadhi ya watu, wanaotaka nafasi hiyo nyeti ambao wengine
hawana sifa na uwezo wa kuwaongoza wananchi.
Kadhalika aliwataka pia kuacha kumshabikia mtu kwa misingi ya
dini au ukabila badala yake watumie utashi wao, unaotokana na uadilifu na
uwajibikaji wao walipokuwa serikalini wakiwahudumia wananchi.
“Nitakapoingia madarakani nitaanza kushughulikia mambo ya
msingi nayo ni wakulima wa mazao ya chakula na biashara, natambua maisha yao
yanategemea sana kilimo hivyo nitahakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na
nje waweze kuuza mazao yao”, alisisitiza.
Alitaja pia kipaumbele kingine ni ujenzi wa viwanda huku
akitolea mfano kilimo cha zao la korosho, suluhisho lake ni kuwajengea wakulima
viwanda vya kubangulia zao hilo ili kuongeza ubora wa zao hilo na kuifanya
jamii, iweze kupata ajira katika viwanda hivyo.
Vilevile alisema atatumia gesi iliyopatikana kwa wingi katika
mkoa wa Mtwara na baadhi ya maeneo mengine ya nchi, kusukuma mbele uchumi wa
nchi yote ya Tanzania bila kubagua na akaongeza kuwa suala hili linahitaji
kiongozi aliyekuwa makini kutokana na kiasi kikubwa cha gesi tuliyonayo hapa nchini.
Pamoja na mambo mengine Waziri Membe amewaahidi
wafanyabiashara kuwa atakapoingia Ikulu ataunda kamati ya wataalamu mbalimbali,
kufuatilia mfumo wa mashine ya EFD’S kama zinamnufaisha mfanyabiashara hasa kwa
wale wadogo wadogo ambao wengi wao licha ya kutumia mashine hizo, bado
inaonekana ni tatizo kwao na kuendelea kuwafanya kuwa maskini.
No comments:
Post a Comment