Mathayo Kaimaima. |
Na Stephano
Mango,
Nyasa.
KADA wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya
Nyasa mkoani Ruvuma, Mathayo Kaimaima ametangaza nia yake ya kuchukua fomu ya
kugombea udiwani katika kata ya Chiwanda wilayani humo, ambayo kata hiyo kwa sasa
inaongozwa na diwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Oddo Mwisho.
Mwisho ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, ameeleza
kuwa wananchi wa kata hiyo wanataka kufanya mabadiliko ya kweli kwa kumpata
kiongozi mwingine wa kutoka chama cha upinzani, ambaye ataweza kuleta ushirikiano
wa karibu katika kusukuma mbele maendeleo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kaimaima alisema
kuwa amechukua maamuzi hayo baada ya kuona kwamba wananchi wake wamekuwa
wakikabiliwa na changamoto nyingi ambazo diwani aliyekuwa madarakani na ambaye
anaelekea kumaliza muda wake, ameshindwa kutatua kero husika na kuwafanya
wananchi waendelee kuwa maskini.
Kaimaima alifafanua kuwa ni jambo la kusikitisha kumuona
Mwisho ambaye amebeba vyeo vingi akiwa pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya
wilaya ya Nyasa, ameshindwa kutetea ujenzi wa barabara ya kutoka Mbamba bay
kwenda mpakani mwa nchi jirani ya Msumbiji ambako ndipo kata hiyo ipo mpakani
humo, na haipitiki na kuwafanya wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla
kushindwa kufanya shughuli zao ipasavyo.
“Barabara hii imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wa kata
ya Chiwanda kutokana na kuwa mpakani, akina mama wajawazito wamekuwa
wakijifungulia njiani kutokana na vyombo vya usafiri kama vile magari hasa
nyakati za masika kukwama wakati mgonjwa anapopelekwa hospitali kwa ajili ya
matibabu”, alisema Kaimaima.
Kada huyo wa CHADEMA ameendelea kumrushia kombora Oddo Mwisho
akisema kuwa, ameshindwa hata kuwaunganisha wananchi ambapo muda mwingi amekuwa
akiwagawa na kujenga makundi, ambayo hayana tija katika jamii kwa manufaa yake
binafsi.
Alisema umefika wakati sasa, viongozi wa CCM kuwapumzisha na
kukipatia nafasi CHADEMA kiweze kuwaongoza wananchi wake kikamilifu, ili waweze
kunufaika na rasilimali zao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake Katibu wa CHADEMA wilaya ya Nyasa, Jacob
Beniwes alisema chama hicho kimejipanga kuwasimamisha wagombea wa udiwani
katika kata zote 21 zilizopo wilayani Nyasa, ikiwemo hata kumsimamisha mgombea
wa ubunge ndani ya wilaya hiyo ambayo ina jimbo moja la uchaguzi.
Katibu huyo alisisitiza kuwa chama kitahakikisha kwamba
kinafanya kampeni zake kwa ustaarabu, usiku na mchana ili kuweza kupata ushindi
mnono ambao utakiwezesha kuongoza wananchi wake wilayani humo na kuwaletea
maendeleo.
No comments:
Post a Comment