Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
MKUU wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho
amesema wakulima waliopo katika wilaya hiyo wanatarajia kupata mavuno mengi
ambayo wameyazalisha katika mashamba yao, katika msimu wa mwaka huu 2015/2016
kufuatia wakulima hao kutumia vyema mvua zilizonyesha na kuzingatia maelekezo
waliyopewa na wataalamu wa ugani wilayani humo.
Nalicho alifafanua kuwa matunda ya kuwa na wataalamu wa
kutosha na wenye kuwajibika kwa wananchi ipasavyo, ndiyo njia pekee iliyochangia
wakulima kuwa na hamasa ya kuzalisha mazao ya biashara na chakula kwa wingi
huku akiwataka watendaji wengine wa idara za Halmashauri wilaya ya Namtumbo,
kuiga mfano huo kutoka kwa wenzao wa idara ya kilimo wilayani humo.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, tangu mpango huo wa kilimo
uanze kuboreshwa hapa nchini, wilaya ilijiwekea mikakati madhubuti ambayo
inatekelezwa na maafisa kilimo kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha kwamba
mazao yanazalishwa kwa wingi na yenye ubora.
Alisema pamoja na kuwepo kwa changamoto mbalimbali wakati wa
utekelezaji wa zoezi la kilimo hicho ikiwemo uzalishaji wa mazao shambani,
anawashukuru watendaji wa vijiji na wataalamu husika kujenga mshikamano na
wakulima, ndio maana leo hii wilaya inajifua kifua mbele kwamba msimu wa mwaka
huu uzalishaji utakuwa mkubwa, jambo ambalo linaleta faraja kwao na kuifanya serikali
kuongeza mapato yake.
Nalicho ambaye amehamishiwa wilaya ya Namtumbo akitokea
Tunduru, kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Rais Jakaya Kikwete kwa baadhi ya
wakuu wa wilaya hapa nchini, aliwapongeza wakulima kwa jitihada walizofanya
kuinua shughuli zao za kilimo.
Mbali na hilo mkuu huyo wa wilaya ameiomba serikali, kuangalia
uwezekano wa kuwa na soko la uhakika la mazao ili kuwaondolea usumbufu wakulima
kutafuta masoko, pale watakapohitaji kuuza mazao yao mara baada ya kuvuna
shambani.
Hata hivyo wilaya ya Namtumbo ambayo ina wakulima wado wadogo,
wengi wamekuwa wakizalisha hasa zao la mpunga, mahindi na matunda hivyo hawana
uwezo wa kutafuta masoko zaidi ya kutegemea wakala wa taifa wa hifadhi ya
chakula, ambaye naye hana uwezo wa kununua kiwango kikubwa cha mazao.
No comments:
Post a Comment