Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
WAKATI serikali ikiendelea na jitihada za kutafuta ufumbuzi
wa kudumu juu ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme katika baadhi ya maeneo hapa
nchini, wakazi na wafanyabiashara waishio katika Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma wamesema tatizo hilo limekuwa sugu kwao kutokana na kukosekana kwa nishati
hiyo muhimu, hivyo serikali inapaswa kulitatua kwa haraka iwezekanavyo, ili
kuweza kuinua uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, mmoja wa
wafanyabiashara ambaye alijitambulisha kwa jina la Said Athuman alisema kwamba
kutokana na kutokuwepo kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Manispaa hiyo
wananchi wanaendelea kuteseka, juu ya uzalishaji wa bidhaa pamoja na shughuli
mbalimbali za kimaendeleo zimeanza kushuka.
Alisema kuwa tatizo hilo limekuwa likilalamikiwa kwa muda
mrefu sasa, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua madhubuti ambayo
itasaidia kumaliza kero hiyo.
Athumani aliongeza kuwa Tanzania ni nchi maskini ambayo bado
inategemea mapato kutoka vyanzo mbalimbali, ambapo kutokana na matatizo kama
hayo yanayoendelea mara kwa mara haiwezi kupata mapato yake ipasavyo, kutokana
na kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa kufuatia kuwepo kwa tatizo sugu la
upatikanaji umeme wa uhakika.
Naye Njelela Haji ameiomba serikali kukubali kubinafsisha
baadhi ya mashirika yake, ikiwemo kwa hili la ugavi wa umeme hapa nchini
(TANESCO) kama ilivyofanya kwa mashirika mengine kwa lengo la kuleta ushindani
utakaosaidia kuongeza uwajibikaji, kwa watendaji wa mashirika ya umma.
Alibainisha kuwa licha ya kero hiyo kuonekana kurudisha nyuma
maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, pia inahatarisha ajira za
watu waliopata vibarua vya kufanya kazi katika viwanda mbalimbali kushindwa
kuendelea kudumu na kuwafanya warudi makwao.
Hata hivyo Kaimu Meneja wa shirika la TANESCO mkoa wa Ruvuma,
Thimoti Ramadhan alikiri kuwepo kwa tatizo hilo la mgawo wa umeme katika
Manispaa ya Songea, huku akiongeza kuwa limesababishwa na kukosekana kwa mafuta
ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
“Tatizo kubwa hapa tulilonalo ni upungufu wa mafuta,
tuliyonayo ni kidogo hivyo tunalazimika kuwasha umeme kwa mgawo, katika baadhi
ya maeneo na baada ya masaa kadhaa tunawasha tena maeneo mengine”, alisema
Ramadhan.
No comments:
Post a Comment